Rubani wa ndege ya shirika la Ethiopia Airlines iliyotua kwa dharura
kwenye uwanja wa ndege wa Arusha, alitua kwenye uwanja huo baada ya
kudhania ni ule wa Kilimanjaro International Airport (KIA), Mamlaka ya
Usafiri wa Anga Tanzania, (TCAA) imesema.
Badala yake rubani huyo alitua kwenye uwanja wa ndege wa Arusha wenye
njia ya kutua iliyo na urefu wa meta 1,640 ambayo ni fupi mno kwa ndege
hiyo aina ya Boeing 767-300ER kutua. Ndege hiyo inahitaji walau njia ya
kutua yenye urefu wa meta 1,798.
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Fadhil Manongi, alisema kwenye maelezo yake
kuwa pamoja na kwamba kulikuwa na ndege mbovu kwenye njia ya kutua ndege
ya KIA, uwanja huo una njia yenye urefu wa meta 3,600 na kusema kuwa
bado kulikuwa na meta 3,200 zilizotosha kwa ndege No. ET-815 kutua.
Amesema tayari wataalam wapo uwanjani hapo kufanya uchunguzi.
Meneja wa Uwanja wa Ndenge wa Arusha, Ester Dede alisema baada ya
abiria wote 213 waliokuwa katika ndege hiyo kusaidiwa na kuendelea na
safari zao, uchunguzi umeanza kubaini chanzo cha tukio hilo.

