Na Mwandishi Wetu
JESHI la Polisi Tanzania, limepeleka timu maalumu ya
askari kutoka makao makuu kwenda wilayani Ulanga, Mkoa wa Morogoro
katika Operesheni ya kuwasaka na kuwakamata baadhi ya wananchi
waliovamia kituo cha Polisi na kukichoma moto pamoja na kuharibu mali
zakituo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, SSP –
Advera Senso, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema
amelazimika kutuma kikosi hicho ili kwenda kuongeza nguvu katika
Operesheni maalumu ya kuwasaka wananchi waliohusika ili sheria ichukue
mkondo wake dhidi yao.
Taarifa inasema timu hiyo maalum ya askari itaongozwa na Kamishina wa
Operesheni na Mafunzo (CP), Paul Chagonja kutoka Makao Makuu ya Polisi.
SSP Senso alisema Jeshi la Polisi linalaani vikali tukio hilo
linaloashiria vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani.
Alisema tukio hilo pia limesababisha vifo na majeruhi pamoja na
kujenga hofu miongoni mwa jamii, ambapo wananchi 3 walipoteza maisha na
wengine 3 walijeruhiwa na kuchomwa moto kituo na malizake.
“Mnamo tarehe 18/12/2013 majira ya saa tatu asubuhi katika kata ya
Malinyi, tarafa ya Malinyi, wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro, kundi la
watu kutoka maeneo mbalimbali kijijini hapo walivamia kituo cha Polisi
Malinyi kwa lengo la kutaka kuwatoa kwa nguvu watuhumiwa 4 waliokuwa
wamekamatwa kwa tuhuma za mauaji.” alisema.
“Katika jitihada za kuhami kituo, askari polisi walitoa tahadhali
mbalimbali za kuwataka wananchi hao watawanyike ikiwemo kupiga mabomu
ya machozi, lakini wananchi hao waliendelea kukaidi amri hiyo. Katika
purukushani hizo za askari kutetea kituo na wavamizi kuendelea kuharibu
mali za kituo ikiwemo kukichoma moto, wananchi 3 walipoteza maisha na
wengine 3 walijeruhiwa,” alisema Senso katika taarifa hiyo.
Aidha, alisema IGP Mwema ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Morogoro
hususani wilaya ya Ulanga kata ya Malinyi, kuwa watulivu na kuendelea
kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi wakati uchunguzi ukiendelea, mtu
yeyote mwenye taarifa za wahalifu hao anaombwa kutoa taarifa kwenye
namba ya simu ifuatayo 0754 78 55 57 au katika kituo chochote cha
Polisi, ili wahalifu hao waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani.
CHANZO:THEHABARI.COM
