Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akizindua mradi wa maji wa Moivaro na Mlangirini
wilayani Arumeru akiwa katika ziara ya siku moja wilayani humo Novemba
19, 2013. Kushoto ni mkewe Mama Tunu Pinda.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na wazee kabla ya kuzindua mradi wa
maji wa Moivaro na Mlangirini wilaya Arumeru akiwa katika ziara ya siku
moja wilayani humo Novemba 19, 2013. . (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amezindua miradi ya maji na umeme wilayani Arumeru
yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 1.8/- ikiwa ni utekelezaji wa
mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now).
Amefanya
uzinduzi huo leo mchana (Jumanne, Novemba 19, 2013) katika vijiji vya
Chekereni na Manyire wilayani Arumeru, mkoani Arusha ikiwa ni sehemu ya
uzinduzi wa miradi kama hiyo katika mkoa mzima wa Arusha.
Akizungumza
na wakazi wa kijiji cha Chekereni, wilayani Arumeru, Waziri Mkuu
alisema katika kutekeleza mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Serikali
imedhamiria kuvipatia maji safi vijiji 271 vya mkoa wa Arusha ifikapo
mwaka 2014.
“Mwaka
2005, ni vijiji 121 tu kati ya vijiji 342 vya mkoa huu ndiyo
vilivyokuwa vikipata maji safi. Mwaka 2012 tulifikisha vijiji 191, na
jinsi tunavyokwenda tunataka tufikie vijiji 271 ifikapo mwaka 2014. Kwa
hiyo tutakuwa tumebakiwa na vijiji 71, na Mungu akijalia tunataraji kuwa
ifikapo mwaka 2015 tuwe tumevikamilisha vijiji vyote,” alisema huku
akisangiliwa na mamia ya wakazi waliojitokeza kushuhudia uzinduzi huo.
Aliwashukuru
wadhamini wa mradi huo wa Chekereni ambao ni kampuni ya Kiliflora kwa
kugharimia ujenzi wa mradi huo lakini akawataka wasiishie hapo bali
waangalie zaidi namna ya kuwasaidia wananchi wajiongezee fursa zao za
kiuchumi.
Kwa
upande wa mradi wa umeme, Waziri Mkuu alimtaka mkandarasi aliyepewa kazi
hiyo kuhakikisha kuwa anakamilisha mradi huo katika muda muafaka na kwa
kiwango cha juu.
“Hatutaki
kusikia visingizio vya sababu za hali ya hewa au sababu za
kijiografia... Miradi hii ni ya gharama kubwa kwa hiyo hatutaki
visingizio. Meneja wa TANESCO hakikisha hakuna visingizio. Kama kazi
hairidhishi, ondoeni huyo mkandarasi, tafuta mwingine,” alisema.
Akisoma
risala kuhusu mradi wa maji wa Chekereni, Mhadisi wa Maji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bibi Joyce Bahati alisema mradi huo
ambao umegharimu sh. bilioni 1.15/-, utawanufaisha wakazi wapatao 16,197
na kupunguza tatizo la maji katika vijiji vya Mlangarini, Moivaro
Olkereian, na maeneo jirani ya Kijenge.
“Mfuko
wa Maendeleo wa Wafanyakazi wa shamba la maua Kiliflora (KWDFL)
umesaidia fedha na jamii imetoa nguvukazi pamoja na ardhi ya ujenzi wa
miundombinu,” alisema.
Alisema
mradi huo ambao ulianza kutekelezwa Septemba 2009, umehusiaha ujenzi wa
kidaka maji; ujenzi wa matanki mawili yenye mita za ujazo 90 kila moja;
ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 15 na utandazaji wa bomba km 21
kutoka kwenye chanzo cha maji chemchem ya Songota.
Mapema
akitoa taarifa kuhusu mradi wa umeme vijijini (REA), Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Bw. George Simbachawene alisema mradi wa kupeleka
umeme vijini katika maeneo ya Manyire kupitia Mlangarini, Seela
Sambashamba, Timbolo, Ilkiding’a na Irkisongo wilayani Arumeru
umegharimu jumla ya sh. 631,440,000/- .
Aliitaja
miradi mingine ya umeme vijijini inayofadhiliwa na Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) ambayo pia inayotekelezwa na TANESCO kuwa ni:- Mradi wa
kupeleka umeme Halmashauri ya Wilaya ya Longido unaogharimu sh. bilioni
1.45/-; Mradi wa kupeleka umeme Mji wa Loliondo Wilaya ya Ngorongoro
ambao gharama yake ni sh. milioni 817/- na Mradi wa kupeleka umeme
Vijiji vya Mto wa mbu Wilayani Monduli ambao pia gharama yake ni sh.
milioni 342/-.
Waziri Mkuu anatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam leo usiku.