Katika hali isiyo ya kawaida, mwanamme mmoja mkazi wa Kijiji cha
Kiria, Kata ya Mamba Kusini, Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro,
anadaiwa kuwabaka na kuwaingilia kinyume cha maumbile watoto wake wawili
wenye umri wa miaka 10 na 13 na kuwajeruhi vibaya.
Mwandishi alivyofuatilia
Ni saa 7:30 mchana nafika nyumbani kwa mwanamme
huyo anayetajwa na baadhi ya watu hapa Moshi kwamba anawabaka watoto
wake.Nabisha hodi, sipati wa kunijibu, baadaye anatokea jirani na
kuniambia wenyewe hawapo, namweleza kilichonileta na anakuwa tayari
kunisaidia.
Jirani huyo ananipeleka kwa msamaria mwema
anayemtunza mtoto wa miaka 13 aliyefanyiwa ukatili na baba yake mzazi
kwa kubakwa na kulawitiwa kwa zaidi ya miaka miwili na nusu sasa nikiwa
njiani anasema “Unapomwangalia mtoto huyo huwezi amini kuwa kitendo hiki
kimetendwa na baba mzazi ambaye bila shaka kabla ya kuwa na watoto
aliomba kwa Mungu na alitamani sana kuwa na watoto naye aitwe baba”
Nafika kwa msamaria huyo katika Kijiji cha Kiria,
Kata ya Mamba Kusini, najitambulisha na kumweleza lengo langu,
ananyanyuka na kuingia ndani kuzungumza na mtoto anarudi na jibu
lililonipa uchungu na kunitoa machozi.
Anamtaja mtoto jina na kusema amesema hataki kuongea na mwanamme, kama unataka mwambie huyo mwanamme atoke hapo nje. Mwanaume anayezungumziwa ni yule ambaye alinisindikiza kuja hapo kumwona.
Anamtaja mtoto jina na kusema amesema hataki kuongea na mwanamme, kama unataka mwambie huyo mwanamme atoke hapo nje. Mwanaume anayezungumziwa ni yule ambaye alinisindikiza kuja hapo kumwona.
Ilinilazimu nimwambie mtu huyo niliyekuwa naye aondoke ili nipate nilichofuata kijijini hapo.
Baada ya kuondoka, mtoto huyo akiwa na uso wa
majonzi alitoka nje na kunisalimia kisha kukaa na kuanza kunieleza
mateso na ukatili wa kutisha aliofanyiwa na baba yake mzazi.
Mateso kutoka kwa baba
Mtoto huyo anasema hakumbuki siku ambayo baba yake
alianza kumbaka lakini anasema ni siku nyingi; mara baada ya baba yake
kutengana na mama yao, zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Anasema baba yake huyo alianza kufanya unyama huo
kwa mdogo wake ambaye sasa ana miaka kumi na baadaye akaanza kumwingia
na yeye na kwamba alikuwa akifanya kwa zamu huku akiwafunga midomo ili
wasipige kelele.
Anasema mara zote alipowafanyia unyama huo alikuwa
na panga pembeni akiwatishia kuwachinja kama watakataa au kusema kwa
mtu yeyote.
Mtoto huyo anaeleza kuwa baba yao alioa mke
mwingine, lakini bado akawa anawaingilia, ndipo siku moja mwanamke huyo
alipomfumania na kupigana nae sana kabla ya kuamua kuondoka na kuachana
naye.
Anasema kitendo cha mama huyo kuondoka kilisababisha baadhi ya
watu kujua ukweli wa matendo ya baba yao, ndipo walipomfuata baba na
kumtaka aache tabia ya kufanya mapenzi na wanaye, baba huyo alikiri
kuwatumia watoto wake wa kuwazaa na kuapa kutorudia tena .
Mtoto huyo anasema hofu ya kuchinjwa ndiyo
iliyomfanya aogope kuwaeleza hata majirani, mdogo wake aliamua kutoroka
kujiepusha na mambo wanayofanyiwa na baba yao.
“Hadi watu kujua nilitoka siku hiyo na kucheza na
wenzangu nje, baba akaja akanikuta,nilipoingia ndani akanikamata na
kunichapa na nondo, sikuthubutu kulia kwa sauti maana alisema
atanichinja. Kwa bahati alipita mama mmoja nje na baba akamwita na
kumwambia nina tabia ya uzururaji lakini yule mama akaanza kumkaripia
baba kuwa kipigo alichonipiga ni kibaya, baba alikasirika na kumfukuza
na kumwambia hajui malezi”
Mara baada ya jirani huyo kuondoka, baba alimpiga
kofi moja ambalo anasema alihisi amezimia, maana hakumbuki
kilichoendelea ila alijikuta kitandani na ilikuwa ni katikati ya usiku,
siku hiyo hakuwa amekula chakula cha usiku.
Huku akitafakari kipigo alichopata na njaa
iliyokuwa inamsumbua, alimwona baba yake akiingia chumbani kwake na
kumvua nguo huku akiwa na panga pembeni, akampaka mafuta ya baby care
sehemu za siri na kisha kuanza kumfanyia unyama wake .
Alipata maumivu makali sana, na baadaye akamgeuza
na kumlawiti kisha akarudia tena, mtoto huyo anasema alishindwa
kuvumilia na kuamua kumng’ata baba yake ambaye alikasirika na kuanza
kumpiga.
Asubuhi iliyofuata alishindwa hata kushuka
kitandani, baba yake alimlazimisha kuamka na kumwambia awashe jiko na
kuchemsha maji ili amkande na baada ya maji kupata moto baba yake
alichukua kitambaa na kumkanda sehemu za siri na kisha kumfunga mkono
aliokuwa amemuumiza kwa kutumia nondo.
“Alivyomaliza kunikanda na kunifunga mkono
aliniambia nisitoke ndani kwa jambo lolote hata kujisaidia nijisaidie
ndani na kuondoka,” anasema mchana jirani aliyemkuta akipigwa usiku
alifika nyumbani hapo kumjulia hali, hakuthubutu kufungua mlango
akihofia baba yake kumkuta na kumchinja”.
Anasema jirani huyo alimwita, alimjibu kuwa baba
yake amemzuia kufungua mlango, mama huyo alikwenda kuwaita majirani
wengine ambao walifungua mlango na kumtoa kisha kumpigia simu mwenyekiti
wa kijiji ashuhudie unyama aliotendewa mtoto huyo.
Majirani wanazungumza
Mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la mama
Jesca anasema wamekuwa na taarifa za muda mrefu kuhusiana na tukio hilo
lakini wanakijiji walishindwa kuchukua hatua kwa kumwogopa.
Anasema mwaka 2012 mwanaume huyo alifumaniwa na
mkewe akifanya mapenzi na mwanaye na ndipo mama huyo alipotoa siri na
wao kama majirani waliungana wakamkamata na kumpa adhabu ya kumchapa
viboko 50 mbele ya wanaume wenzake na kurudi nyumbani lakini baada ya
siku chache alirudia kuwatendea ukatili wa kutisha watoto hao.
Anasema baada ya yeye kuanza tena unyama dhidi ya watoto wake
walipeleka taarifa kwa kiongozi mmoja wa kanisa ambaye aliitisha kikao
na viongozi wa vijiji na ukoo wao kuzungumzia jambo hilo ambapo mwanaume
huyo alikiri na kuapa kutorudia tena.
Mwenyekiti wa kijiji
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiria, Doroth Mtui,
anasema baada ya kupata taarifa kutoka kwa majirani wa watoto hao,
alilazimika kufika nyumbani kwa mtuhumiwa kuzungumza na mtoto huyo ambae
alimweleza ukatili anaofanyiwa na baba yake, na ndipo alipopiga “ yowe”
kuita wananchi wengine ambao waliandamana kwa pamoja kumkamata mwanaume
huyo,na kumpeleka Kituo cha Polisi Himo.
Baada ya kufika kituo cha polisi Himo, walitakiwa
kumpeleka mtoto huyo hospitalini, ili kuthibitisha kama kweli amebakwa,
taarifa iliyotolewa na daktari wa Hospitali Teule ya Kilema, ilionyesha
kuwa mtoto huyo ameingiliwa sehemu zote mbili, na kwamba ni kitendo cha
muda mrefu kilichosababisha kuota nyama sehemu zake za siri.
Uongozi wa kanisa analosali
Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Usharika wa Rauya, Mchungaji Anayesu Ringo alikokuwa anasali
mwanamme huyo alikiri kufanya kikao na familia ya mtuhumiwa na kukiri
kuishi na wanawe, aliomba kusamehewa na kanisa kushauri watoto hao
kwenda kuishi na bibi yao na sio kulala nyumba moja na baba yao.
Mchungaji Ringo anasema anashangaa kusikia bibi
aliwarudisha wajukuu zake, kwenye mateso hayo, na kusema jamii inapaswa
kutambua kuwa jukumu la kuwatunza watoto ni la jamii nzima, familia
inapaswa kutambua kuwa malezi bora yanaanzia ngazi ya familia.
Wanaukoo wanasemaje?
Mmoja wa wanaukoo (jina tunalo), anasema wao kama
wanaukoo walishakaa na kumuonya ndugu yao lakini ni mkorofi na
hamsikilizi mtu na kwamba ukorofi wake ulisababisha kila mtu kumwacha
aishi anavyotaka.
“Huyu ndugu yangu ameonywa sana lakini hasikii
wanawake waliungana hapa na wakamchapa viboko ,mchungaji alimwita
ofisini tukajadili jambo hili na kukiri kuacha na sisi tuliamini
ameacha, kumbe anaendelea na tabia hii ya uhayawani,” anasema.
Taarifa ya daktari
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Dk S. Berna
wa Hospitali Teule ya Kilema mashavu ya sehemu za siri (labia) yana
maambukizi na kwamba ana kidonda.
Ripoti pia inaonyesha kuwa licha ya umri wake kuwa mdogo, mtoto
huyo si bikira, jambo ambalo kwa umri huo sio rahisi mtoto kuwa hivyo .
Taarifa hiyo pia inaonyesha sehemu za siri za
mtoto huyo zinatoa majimaji yasiyo ya kawaida yanayoashiria maambukizi
sehemu za uzazi huku njia ya kutolea haja kubwa ikiwa imeathiriwa
vibaya kutokana na misuli yake kulegea.
Mtaalamu wa watoto anasemaje
Mtaalamu wa masuala ya watoto kutoka Hospitali ya
Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi, Saganda Kapalala anasema mtoto
anapofanyiwa ukatili, hupata madhara mbalimbali ambayo huweza kuathiri
maisha yake yote.
Saganda anasema madhara apatayo mtoto aliyebakwa
ni pamoja na kuathirika kisaikolojia na kuwaona wanaume kuwa watu katili
na hata baadaye anaweza asiolewe tena kutokana na kukosa imani na
wanaume.
Maoni ya Wanaharakati
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake (Tamwa), Valery Msoka akizungumza na mwandishi wa makala haya
anasema ni jambo la kusikitisha kuona mtoto anafanyiwa ukatili wa
kinyama namna hii lakini ukafumbiwa macho kwa muda mrefu.
Naye Elizabeth Minde ambae ni Mkurugenzi wa
Shirika lisilo la Kiserikali linalojihusisha na Utetezi wa Haki za
Binadamu Jinsia na Watoto (kwieco) amelaani kitendo hicho na kusema
kamwe hawatalala hadi haki itendeke.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz
alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba wameshamkamata mtuhumiwa,
atafikishwa mahakamani wakati wowote uchunguzi utakapokamilika.
Kamanda Boaz anasema jambo hili limemsikitisha
sana kutokana na ukweli kwamba mzazi ndiye alipaswa kuwa mlinzi wa
familia, sivyo kama ambavyo sasa anatuhumiwa kwamba amekuwa akiwaharibu
watoto wake.
“Huyu mtu tuko naye, tumemkamata, bila shaka
sheria itachukua mkondo wake, lakini kwa kweli ni jambo
linalosikitisha,” anasema Kamanda Boaz.
CHANZO:MWANANCHI
CHANZO:MWANANCHI
