Siku moja baada ya
wabunge kuwataka Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na
Utalii, Khamis Kagasheki kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia Operesheni
Tokomeza Ujangili, meno 706 ya tembo yamekamatwa jijini Dar es Salaam.
Meno hayo 706 ni
sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi za wanyama pori mbalimbali
hapa nchini. Tukio hilo lililotokea jana jioni katika Mtaa wa Kifaru,
Mikocheni, wilayani Kinondoni, liliongozwa na Waziri Kagasheki ambaye
aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tarish
Maimuna.
Waliokamatwa na
shehena hiyo ya meno ya tembo ni raia watatu wa China ambao ni Xu Fujie,
Chen Jinzha na Huang Qin wote kutoka mji wa Guandung .
Raia hao wa China
wamekuwa wakiishi katika nyumba hiyo kwa miaka mingi wakifanya biashara
ya kuingiza nchini vitunguu swaumu kutoka China na kusafirisha nje ya
nchi makombe yanayopatikana baharini.
Alipoingia ndani ya
nyumba hiyo, Kagasheki ambaye aliambatana na askari polisi na baadhi ya
maofisa usalama alishuhudia shehena kubwa ya meno ya tembo ikiwa
imehifadhiwa kwenye viroba vyenye uzito wa kilo 50.
Mbali ya kushuhudia
shehena ya meno hayo, alionyeshwa gari maalumu aina ya Toyota Noah
ambalo watuhumiwa hao hulitumia kutoa pembe porini na kuyaingiza jijini
Dar es Salaam.
Akizungumza katika
eneo la tukio mara baada ya kuwakamata alisema kukamatwa kwa watu hao
kunatokana na matokeo ya Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo imesitishwa
na Serikali juzi baada ya wabunge kuilalamikia.
Waziri Kagasheki
alisema kwamba katika harakati za kutaka kuwakamata watuhumiwa hao
walitoa Sh30 milioni kwa ajili ya kujaribu kuwahonga askari.
“Walitaka kuwahonga askari ili wasikamatwe,” alisema huku akionyesha noti za fedha hizo.
Alisema wabunge
wanaomtaka ajiuzulu kwa madai kwamba Operesheni Tokomeza Ujangili
imesababisha mauaji ya watu na mifugo wanapoteza muda kwa kuwa mwenye
mamlaka ya kumtoa ni Rais Jakaya Kikwete pekee.
“Sasa mimi nasema kunitoa haitakuwa rahisi anayeweza kunitoa ni yule aliyeniweka,” alisema.
Alisema ipo mikakati inayofanywa na baadhi ya wabunge kutaka kuwang’oa baadhi ya mawaziri kwa masilahi binafsi ya kisiasa.
“Itakuwa ni jambo
la ajabu kwamba kila mtu akiingia madarakani wanataka atoke, watatolewa
wangapi?” alihoji na kuongeza kuwa operesheni hiyo ni muhimu kwa ajili
ya kunusuru tembo wasiishe.
Alisema kwamba ni
kweli kuna baadhi ya dosari zimejitokeza kwenye operesheni ikiwamo
kuuawa kwa baadhi ya mifugo, lakini siyo kwamba zoezi zima halina
manufaa.
Kagasheki alisema kama kasi hii ya kuuawa kwa tembo itaachiwa iendelee baada ya miaka 10 tembo wote watakuwa wameisha nchini.
Alisema hataki kuona utawala wa Rais Kikwete ukiondoka madarakani ukiwa na lawama ya kuachia majangili wawamalize tembo.
Mmoja wa watuhumiwa
hao, Huang Qin alisema shehena yote ya meno ya tembo iliyokamatwa
nyumbani kwake ilikuwa ikiletwa kidogo kidogo na rafiki yake ambaye
hakumtaja jina.
Akiongea kwa Kiswahili Qin alisema: “Mimi hii si yangu, kichwa yangu mbovu. Rafiki yangu alileta hii (meno) kidogo kidogo.”
Januari mwaka huu,
Gazeti La Daily Mail la Uingereza liliripoti kwamba Serikali ya Kenya
imekamata shehena ya vipande 638 vya meno ya tembo ambavyo ni sawa tembo
320 waliouawa.
Mzigo huo wa tani mbili ulikuwa kwenye kontena la mawe ya urembo (marumaru) kutoka Tanzania.
Taarifa zaidi
zinaonyesha kuwa tani nne za meno ya tembo yenye thamani ya Dola za
Marekani 3.4 milioni sawa na takriban Sh5.4 bilioni zilikamatwa Hong
Kong Oktoba 20, mwaka jana, huku ikielezwa kuwa meno hayo yalikamatwa
yakisafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.
Agosti 16 mwaka huu
polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam, walimkamata raia wa Vietnam akiwa na meno ya tembo yenye thamani
ya Sh18.4 milioni yaliyotengenezwa kama bangili tayari kusafirisha
kwenda nje ya nchi.
Chanzo: Mwananchi
