Mahakama ya Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, imewaachia huru
vigogo watano wa halmashauri ya wilaya hiyo, waliokuwa wakikabiliwa na
mashtaka ya uhujumu uchumi.
Kesi hiyo ilifunguliwa Juni 13 mwaka huu na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) iliyokuwa
ikiwatuhumu vigogo hao kuisababishia halmashauri hasara ya Sh29.9
milioni.
Hukumu ya kuwaachia huru washtakiwa hao waliokuwa
wakitetewa na wakili Duncan Oola wa jijini Arusha, ilitolewa Ijumaa
iliyopita na Hakimu wa Wilaya ya Rombo, Yohana Myombo.
Walioachiwa huru na nyadhifa zao zikiwa kwenye
mabano ni Joseph Ngoseki (Ofisa Elimu), Emmanuel Masele (Mweka Hazina)
na Elias Mshana, (Kaimu Mkurugenzi).
Wengine ni Erick Barongo (Mhasibu) na Rahel Mshangila (Ofisa Ugavi Msaidizi.
Katika hukumu yake, Hakimu Myombo alisema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka hayo.
Juni mwaka jana, Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Maghella Ndimbo, alidai kuwa makosa yalitendeka Septemba mwaka 2007.
Na Daniel Mjema, Mwananchi
Na Daniel Mjema, Mwananchi
