Na Mohamded Mhina wa Jeshi la Polisi, Zanzibar
Mzee mmoja mwenye umri wa miaka 55, mkazi wa Kijiji cha Kidutani Gando
mkoa wa Kaskazini Pemba ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka mtoto
mwenye umri wa miaka 12 na baadaye kujitosa bahari kukwepa mkono wa
dola.
Mzee huyo Muslih Mserembe, alikamatwa na wananchi waliokuwa
wamekizingira kibanda chake kilichojengwa kwa miti, kuezekwa kwa makuti
na kukandikwa kwa udongo wakati akimbaka binti huyo bila ya huruma.
(Jina la binti huyo linahifadhiwa kwa usalama).
Kamishna wa Polisi Zanzibar CP Mussa Ali Mussa(Pichani), amesema kuwa tukio
hilo limetokea jana majira ya saa 12.00 alfajiri wakati binti huyo
akiwafuatilia wenzake kwenda shambani kuokota maembe na ndipo mzee huyo
alipomuona na kumuita
Amesema baada ya binti huyo kumsogelea mzee huyo, alimwambia waingie
ndani ya nyumba yake akidai kuwa angempatia maembe badala ya kuwafuata
wenzake na ndipo alipombaka na binti kupiga kelele za kuomba msaada.
Kamishna Mussa alisema baada ya kelele hizo wananchi walikwenda
nyumbani kwa mzee huyo na wakati wakiizingira nyumba yake, mzee huyo
alitoka na kutimua mbio na kwenda kujitosa baharini lakini wananchi nao
walijitosa humo na kumvua kama samaki.
Amesema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo, wananchi hao walimpeleka
katika kambi moja ya KMKM na ndipo Polisi walipofika na kumchukua kwa
hatua zaidi.
Kamishna huyo wa Polisi Zanzibar amesema kuwa binti aliyebakwa
alikimbizwa katika Hospitali ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba kwa
matibabu zaidi na hali yake imeelezwa kuendelea vizuri.
Kamishna Mussa ambaye amelaani vikali kitendo hicho, lakini amepongeza
hatua za wananchi za kumkamata mtuhumiwa bila ya kumzuru na kumfikisha
kwenye vyombo vya dola akiwa salama.
Mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani kujibu shitaka lake.