ATUPWA JELA MIAKA 30 KWA UNYANG'ANYI WA PIKIPIKI

Drug-Lord-Found-Dead-In-Jail-Cell
Na Nathaniel Limu, Singida via moblog

Kijana mkulima mkazi wa kijiji cha Mkenene kata ya Mugungira Wilaya ya Ikungi mkoani Singida,Daud Melembeka  (22)amehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Singida adhabu ya kutumikia jela miaka 30 baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kunyang’anya pikipiki kwa kutumia silaha aina ya nondo.

Mapema Mwendesha Mashitaka Sajenti wa Polisi,Godwel Lawrance alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Singida,Flora Ndale,kuwa mnamo novemba 14 mwaka jana huko maeneo ya karakana manispaa ya Singida,bila halali mshitakiwa Daud alimnyang’anya Emmanuel Mussa pikipiki T.914 CCS aina ya fekon,huku akijua wazi kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Mwendesha Mashitaka huyo amesema kabla na baada ya kufanya unyang’anyi huo,mshitakiwa Daud alimtisha na kumpiga mlalamikaji Emmanel kwa nondo,ili kumwogofya aweze kutekeleza lengo lake hilo bila matatizo.

Amesema siku ya tukio mshitakiwa alikodisha pikipiki hiyo na wakati wanaendelea na safari,ghafla mshitakiwa alimwamuru dereva Emmanuel asimamishe pikipiki na ndipo alipopata fursa ya kupora pikipiki hiyo.

Hata hivyo,Lawrance amesema kesho yake novemba 15 mwaka jana saa nane mchana mshitakiwa Daud aliweza kukamatwa na askari polisi E.81 D/CPL Masoye akiwa Manyoni mjini na pikipiki aliyompora mlalamikaji Emmanuel.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo,Mwendesha Mashitaka Lawrance amesema mshitakiwa Daud ni kijana mdogo mwenye nguvu za kutosha kumwezesha kufanya kazi halali ambazo zinaweza kumpatia kipato cha kukidhi mahitaji yake muhimu,lakini ameamua kutumia njia isiyo halali katika kujiingizia mapato.

“Ili iwe fundisho kwa mshitakiwa na iweze pia kuwaogofya watu wengine wanaotarajia kufanya makosa ya unyang’anyi kwa kutumia silaha,naiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshitakiwa”,amesema.

Akitoa hukumu hiyo,hakimu Ndale amesema kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka,umethibitisha bila kuacha chembe chembe ya shaka kuwa mshitakiwa anayo hatia kama alivyoshitakiwa.

“Makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha,sheria imetamka wazi kwamba adhabu yake ni miaka 30 jela.Kwa hiyo utatumikia jela miaka 30 ili iwe fundisho kwako na watu wengine wanaotarajia kufanya makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha”,amesema hakimu Ndale.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo