Polisi nchini Somalia walivamia makao makuu ya kituo
cha redio cha Shabelle, na kukilazimisha kufunga matangazo yake mnamo
siku Jumamosi.
Maafisa wakuu wanasema kuwa wanadhibiti jengo hilo ambalo lilikuwa linamilikiwa na serikali miaka ya nyuma.
Kituo hicho kinasifika kwa kukosoa sana maafisa wakuu wa serikali.
Hatua ya kudhibiti jengo la kituo hicho, ni ya
hivi karibuni katika mfululizo wa mashambulizi dhidi ya waandishi huru
wa habari ambayo yamekuwa yakifanywa na serikali sawa na kundi la
kigaidi la al-Shabaab.
Kituo hicho hata hivyo kiliwahi kutakiwa kuondoka katika jumba hilo.
Maafisa wa usalama wanasema kuwa notisi ya siku
tano waliyotoa kwa wakuu wa kituo hicho kuwataka kuondoka katika jumba
hilo imefika mwisho lakini wakuu wa kituo hicho wanasema kuwa
wanakodisha jumba hilo kihalali kwa mujibu wa mkataba waliokuwa nao na
serikali iliyotangulia.
Serikali ya Somalia iko katika harakati ya kumiliki majengo na taasisi zilizokuwa zinamilikiwa na serikali ya awali.
Wanaharakati wanasema kwua hatua hii itahatarisha maisha ya waandishi wa habari, wengi wanaoishi katika jengo hilo.
Radio Shabelle iliripoti kwenye mtandao wake
kuwa polisi waliingia katika jengo hilo kwa lazima na hata kuwachapa
baadhi ya waandishi waliokuwa kazini.
Walioshuhudia tukio hilo walifahamisha shirika
la habari la AFP kuwa wafanyakazi wa rediao hiyo walionekana wakiwekwa
ndani ya lori za polisi kwa nguvu.
Hata hivyo polisi walikana kuwa operesheni yao
ilikuwa inalenga shughuli za kituo hicho kwani kinasifika sana kwa kuwa
wakosoaji wakuu wa serikali.
Waziri wa mambo ya ndani anasema kuwa jengo hilo
lilikuwa ofisi za shirika la ndege la Somalia na kwa hivyo basi
linapaswa kurejeshwa kwa serikali.
Aidha wakuu wa kituo hicho wanasema kuwa
walikuwa wanatumia jengo hilo lililokaribu na uwanja wa ndege kihalali
baada ya makubaliano kati yao na serikali ya awali.
Waandishi wa habari nchini Somalia ni baadhi ya
wanaokabiliwa na tisho kubwa la usama dhidi ya maisha yao kama
waandishi, hii ni kwa mujibu wa shirika la waandishi wasio na mipaka.
Waandishi habari 18 waliuawa nchini Somalia
mwaka 2012 huku shirika hilo likisema kuwa waandishi 10 wa Redio
Shabelle wameuawa tangu mwaka 2007.