MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO AONGOZA MAMIA KUMZIKA KAMANDA JAMES KOMBE

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama, amewaongoza Maelfu ya  waombolezaji katika mazishi ya Aliyekuwa Mkuu wa kitengo cha Usalama  Barabarani, Kamishna mstaafu, James Kombe (63), aliyefariki dunia  October 21 mwaka huu katika Hospitali ya Ocean Road, jijini Dar es  salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Kombe aliyeitumikia Jeshi la Polisi kwa muda wa miaka 24, katika  nyadhifa mbalimbali, alizikwa jana saa 9:40, alasiri, Nyumbani kwake  katika kijiji cha Msae, kata ya Mwika, Jimbo la Vunjo, wilaya ya Moshi  vijijini, mkoani Kilimanjaro baada ya ibada ya maziko iliyofanyika  katika Usharika wa Msae-Lyakrimu na kuongozwa na Askofu Mkuu wa KKKT,dayosisi ya Kaskazini, Dkt. Martin F. Shao.

Akitoa Salamu za Rambirambi, Gama alisema serikali imeguswa na msiba  huo huku akimuelezea Marehemu Kombe kama mtu muadilifu, mwaminifu na  mtu asiyekuwa, asiyekuwa na ubinafsi na mzalendo aliyeitumikia Taifa  lake kwa nguvu zake zote hadi dakika za mwisho za uhai wake.

“Ni kweli mazingira yetu kikazi yanatofautiana, lakini ni wazi kuwa  kuna mengi ya kujifunza na kujivunia kutoka kwa Kamishna Kombe enzi za  uhai wake, Marehemu ameacha historia iliyotukuka nyuma yake, alikuwa  ni mtu mwadilifu sana, mwaminifu, mzalendo na mchapa kazi  aliyejitoleakulitumikia Jeshi la Polisi na Taifa kwa ujumla,” alisema Gama.

Kuhusu swala la uwajibikaji na utendaji kazi, Gama alisema wananchi  wengi kwa sasa wanashindwa kufanya kazi za maendeleo hasa mkoani  Kilimanjaro katika maeneo ya Rombo, Marangu na Mwika kutokana na  kukithiri kwa vitendo vya Unywaji pombe holela ambapo aliagiza wakuu  wa wilaya kuhakikisha wanasimamia na kudhibiti hali hiyo.

Awali akiongoza Ibada ya Maziko, Askofu MKuu wa KKKT, dayosisi ya  Kaskazini, Dkt.  Martin Shao, aliwataka waumini wa dini ya Kikristo, wananchi pamoja na  watumishi katika Jeshi la Polisi kufanya yale yaliomema ikiwa kweli
wanataka kuenziwa kama ilivyo kwa Marehemu Kombe.

Dkt. Shao katika ibada hiyo alimuelezea Marehemu Kombe kama mtu  anayestahili kuenziwa daima kama anavyoenziwa Hayati Baba wa Taifa,  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutoka na utendaji wake kazi  uliotukuka, uzalendo na Uadilifu pamoja na uwajibikaji katika  kuhakikisha Amani ya Tanzania na usalama wa Wananchi wake.

Kabla ya kifo chake, Kamishna Kombe, alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa  wa Kansa ambao ulianza kumsumbua Juni mwaka jana na kutibiwa katika  Hospitali ya Rufaa KCMC mjini Moshi.

James Kombe, aliyezaliwa mwaka 1950, mwika Kilimanjaro ameacha mjane mmoja, Maria Kombe na watoto watano na kwamba alilitumikia Jeshi la polisi kuanzia Machi, mwaka 1970 na kulitumikia mpaka alipostaafu mwaka 2010.

Akisoma historia ya Marehemu, Kamanda wa kikosi cha usalama Barabarani, Joseph Mwakabonga alisema Kamishna Kombe, alijiunga na Mafunzo ya awali machi 23 mwaka 70 na kumaliza Agosti 28 mwaka huo, huko Moshi baada ya kuhitimu elimu ya sekondari mwaka 1969 nchini Uganda.

Alisema alipandishwa vyeo kama Mkaguzi wa polisi (1977), Kamishna msaidizi (1995), Mkaguzi wa polisi (1986), mrakibu mwandamizi (1991) na Kamishna Msaidizi wa Polisi (2002) hadi alipostaafu 2010.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo