ASKOFU Mkuu wa kanisa la Redeemed Gospel nchini Kenya Arthur Kitonga amepinga wito wa baadhi ya mapasta kutaka serikali iwape bunduki ili kujikinga kutokana na mashambulizi katika makanisa.
Akiongea na Taifa Leo
kwa njia ya simu kutoka Amsterdam Jumanne, Askofu Kitonga alikariri
msimamo wa kanisa lake kuhusu suala hilo ambalo limezua mjadala katika
vyombo vya habari huku wananchi wengi wakionekana kutofurahia pendekezo
la mapasta.
Mashambulizi
ya mara kwa mara na watu wasiojulikana hasa katika sehemu za Mombasa na
Kilifi yamepelekea kuuawa kwa mapasta wawili hivi majuzi akiwemo pasta
wa Kanisa la Redeemed kwa jina Charles Matole.
Katika
mazishi ya Pasta Matole, viongozi wa makanisa waliilaumu serikali kwa
kutowalinda vilivyo na kuitaka Serikali iwape bunduki aina ya AK47 ili
wajikinge kutokana na mashambulizi ya adui.
Askofu
Lambert Mbela ambaye ni Kiongozi wa kanisa la Redeemed Gospel eneo la
Pwani Kaskazini alinukuliwa akiitaka serikali iyakabidhi makanisa
bunduki aina ya AK47.
Lakini hapo Jumanne Askofu Kitonga alipinga jambo hilo na kusema huo sio msimamo wa kanisa.
“Tunapiga jambo la watumishi wa Mungu kupewa bunduki. Jambo hilo halifai,”akasema Askofu Kitonga kwa njia ya simu.
Askofu huyo
mkuu aliahidi kutoa maelezo zaidi kuhusu jambo hilo pindi tu
atakaporejea nchini kutoka kwenye ziara yake ya Australia.
Mwito wa
mapasta kujihami umezua mjadala mkali kwenye vyombo vya habari huku
wengi wakisema ni kinyume na mafundisho ya Biblia na maandili ya
Kikristo.
“Kama
Wakristo hatufai kumwaga damu. Mwito wa mapasata kupewa bunduki una
maana watatumia bunduki hizo kuua kinyume na amri kumi za Mungu,”akasema
shabiki mmoja huku akichangia kwenye mjadala katika kituo kimoja cha
Redio Jumanne.
Wengi wa
waliochangia katika mjadala huo walinukuu maandishi matakatifu
yanayopendekeza kutolipiza kisasi na kumwachia Mungu kupambana na maadui
zao.
Amri za Mungu
Mnamo wiki
jana Askofu Kitonga pamoja na viongozi wengine wapatao 200 kutoka kwa
madhehebu mbalimbali ya Kiijilisti walikutana mjini Nyeri na kutoa
mwito kwa serikali izidishe usalama katika makanisa.
Viongozi hao
wa makanisa walisikitishwa na ukosefu wa usalama nchini na makanisani
na wakaitaka serikali ichunguze wageni walioko nchini kunyume cha
sharia huku wakisema huenda wageni hao ndio wanaosababisha visa vya
uhalifu kuongezeka.
Hata hivyo,
Askofu Kitonga na wenzake hawakuitisha bunduki mbali walisema ni jukumu
la serikali kuwalinda wananchi wote ikiwepo ni pamoja na viongozi wa
makanisa.
Vile vile
viongozi hao wa makanisa waliwataka wakristo kuwa na uvumilivu na
kutowalaumu waislamu kwa mashambulizi ya makanisa huku wakisema kwamba
mashambulizi hayo yalitekelezwa na ‘watu wachache wenye msimamo mkali’
na wala si Waislamu.