WAANDISHI WA HABARI WAONYWA KUTOINGILIA UHURU WA MAHAKAMA

Picture
Jaji Kiongozi Fakihi AR Jundu akionesha kwa waadishi gazeti la Jamuhuri la toleo la Agosti 27- Septemba 2 lenye kichwa cha habari "Majaji wanaolinda wauza 'unga' wabainika".
Imeandikwa na  Eliphace  Marwa, Dar es Salaam - JAJI  Kiongozi wa Mahakama Kuu Tanzania  Fakih Jundu amewaasa waandishi wa habari kuwa makini pindi wanapoandika habari zinazohusu mahakama ili kuondokana na tatizo la kuingilia uhuru wa mahakama.

Hayo yamesemwa Jana jijini Dar es salaam na Jaji Kiongozi  Fakih alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake kufuatia taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la kila wiki linalotuhumu muhimili huo kwa kushindwa kuwachukulia hatua stahiki watuhumiwa wa kesi za madawa ya kulevya.

"Huku ni kutaka kupambanisha wananchi na mahakama yao ambayo wana imani nayo, ni vyema waandishi kupata ufafanuzi wa kina wa mambo mbalimbali kabla ya kuandika habari isiyo ya kweli na yenye lengo la kupotosha Umma", alisema Jaji Fakih.

Aidha Jaji Fakih aliongeza kuwa ni vema kwa waandishi wa habari kuwa makini na uandishi wa habari zinazohusu mahakama kwa kuwa na ushahidi wa kutosha kwani kwenda kinyume na hapo ni kuingilia uhuru wa mahakama na si vizuri kwa waandishi wenye ueledi kuandika habari kwa ushabiki.

"Mengi ya mashauri yaliyotajwa na gazeti hilo bado yako mahakamani hivyo si vyema kuingilia uhuru wa mahakama hivyo habari hii inapaswa kukemewa kwa kosa la kuzungumza mambo yaliyo mahakamani", aliongeza Jaji Fakih.

Akizungumzia suala la kuwepo mahakama maalumu zitakazosimamia kesi za dawa za kulevya Jaji Kiongozi huyo amesema kama itaundwa na kuwezeshwa vizuri zinaweza kufanya kazi ila kama hazitawezeshwa kwa kupatiwa fedha na rasilimali watu hazitaweza kufanya kazi ipasavyo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo