Serikali wilayani Makete mkoa wa Njombe imetolea ufafanuzi wa sakata la nyumba za ibaada kujengwa katikati ya makazi ya watu, hali inayosababisha kero kwa baadhi ya watu wanaozunguka maeneo hayo
Hivi karibuni kumeibuka minong'ono na manung'uniko miongoni mwa wakazi wa makete mjini wakilalamikia kero wanazozipata kutoka kwenye baadhi ya nyumba za ibaada kufanya ibaada hata usiku kwa kusikika sauti za muziki pamoja na nyimbo kutoka kwenye nyumba hizo hali inayopelekea wengi wao kushindwa kulala wawapo majumbani mwao
Ufafanuzi huo umetolewa hii leo na Afisa ardhi wilaya ya Makete Anikasi Anzela wakati akizungumza na waandishi wa habari na kukiri kuwa ni kweli kumekuwa na utitiri wa nyumba za ibaada zinazoleta kero kwa watu hasa kwa nyumba hizo kuwepo kwenye makazi ya watu
Amezitaja sababu zinazopelekea nyumba hizo kujengwa kwenye makazi ya watu kuwa ni pamoja na kujenga nyumba hizo bila kuiona ofisi yake pamoja na afisa mipango miji ili awaelekeze sehemu ya kujenga kanisa ama msikiti, pamoja kukwepa kulipia gharama za kiwanja zilizowekwa kwa mujibu wa sheria
"Unakuta watu wanakwepa kulipa gharama za kiwanja, kwa hiyo wanaoka ni pesa nyingi, unakuta miongoni mwao yupo muumini mwenye kiwanja hivyo anaamua kukitoa bure ili ujengwe msikiti ama kanisa na kwa kuwa mtu huyo alipewa kiwanja kwa ajili ya kujenga nyumba ya kuishi basi utashangaa inajengwa nyumba ya ibaada, kwa vyovyote vile hili suala lazima lilete kero kwa watu" alisema Anzela
Katika hatua nyingine Afisa ardhi huyo ameitaka jamii kutoa taarifa ofisini kwake pale wanapopata usumbufu wa sauti zinazotoka kwenye nyumba za ibaada, pamoja na nyumba za watu binafsi ama za starehe ambazo zinaleta usumbufu kwa wananchi ili hatua zichukuliwe mara moja