MWAMUZI WA MECHI YA YANGA NA COASTAL UNION KUFUNGIWA MSIMU MZIMA

Mwamuzi Martin Saanya (katikati) akiwa na waamuzi wenzake baada ya mechi ya Yanga dhidi ya Coastal Union.

Na Khatimu Naheka
TAARIFA kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinasema mwamuzi aliyechezesha mechi ya Yanga dhidi ya Coastal Union, Agosti 28, mwaka huu, Martin Saanya, anaweza kufungiwa kuchezesha msimu mzima.
Viongozi wa Kamati ya Ligi Kuu Bara mpaka jana walikuwa hawajapata ripoti ya kamisaa wa mchezo huo, lakini inaelezwa wameangalia baadhi ya matukio ya mchezo huo kwenye CD na kubaini makosa makubwa kwa upande wa mwamuzi.

Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara ilichezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya 1-1. Coastal walipata penalti dakika ya 90 mwamuzi akidai beki David Luhende aliunawa mpira kwenye eneo la hatari. Hali hiyo ilizua utata wengi wakidai haikuwa penalti halali.

Mmoja wa mabosi wazito ambaye yupo ndani ya Kamati ya Ligi, ameliambia Championi Jumatatu kuwa, tayari maafisa kadhaa wa Kamati ya Waamuzi wameona upungufu mwingi wa Saanya katika mechi hiyo.

Kigogo huyo alisema CD inaonesha kwamba Saanya alishindwa kutafsiri vizuri baadhi ya matukio huku pia akionekana kuwa na kasoro ya kutokuwa sehemu sahihi wakati wa mchezo, jambo ambalo ni kosa.

Bosi huyo ambaye ameomba hifadhi ya jina lake, amesema kwa sasa bado hawajakutana kujadili ripoti ya mchezo huo, lakini akasisitiza uchunguzi wa awali unaonyesha Saanya ana makosa yanayoweza kusababisha afungiwe msimu mzima.

 “Ukifuatilia viongozi wake (Saanya) wa waamuzi wanasema kwamba hakuwa katika maeneo sahihi kulingana na matukio kadhaa ya mchezo, wanasema waamuzi wanashauriwa kuhakikisha wanaweza kufika katika maeneo ambayo mpira upo, kitu ambacho Saanya hakufanya, sasa hilo pekee linaweza kumuweka katika wakati mgumu,” alisema bosi huyo mzito ndani ya kamati hiyo.

Championi Jumatatu lilipomtafuta mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia, alisema kwa sasa bado wanasubiri ripoti ya mchezo huo itakayojadiliwa pamoja na ripoti nyingine za michezo iliyopita na baada ya hapo maamuzi yatatolewa.

CHANZO: CHAMPIONI


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo