Sehemu ya mji wa Nyeri.
MSHUKIWA wa wizi wa mabavu Ijumaa aliomba mahakama ya Nyeri kuharakisha kusikizwa kwa kesi yake huku akilalamika wingi wa chawa kwa jela haswa wakati wa msimu huu wa baridi.
Hakimu mkuu
wa Nyeri, Bi Wilbroda Juma alishtuliwa na madai ya Maina na kumuamuru
afisa wa polisi kuhakikisha kuwa ameweza kuchunguza kwa makini madai
hayo ya wafungwa kuumizwa na chawa.
Joseph Maina aliomba mahakama iweze kuharakisha kuisikia kesi hiyo kwani anaumia sana akiwa kwenye rumande.
“Imefika miaka miwil sasa na kesi yangu bado haijasikizwa,” aliteta Bw Maina.
Maina
ameshtakiwa pamoja na Duncan Mumangari na James Ngunjiri kuwa mnamo siku
ya Julai 7, mwaka jana walimuibia Bw James Macharia simu na pesa
taslimu zote zikiwa ni za thamana ya Sh14,000 katika kijiji cha Ruring’u
katika eneo la Nyeri.
Watatu hao pia wanashtakiwa kumuumiza Bw Macharia kwa kutumia silaha kama vile rungu.
Bi Juma
alimhakikishia Maina kuwa mahakama hiyo imeyasikia malalamiko yake na
kueleza kuwa kesi imechukua muda mrefu kusikizwa kwani mwendesha wa
mashtaka anatafuta uchunguzi kamili kama vile washahidi na ripoti ya
daktari kuthibitisha kuwa kwa kweli mlalamishi alikuwa ameumizwa.
“Kesi yenu itasikizwa haraka iwezekanavyo mnamo siku ya Septemba 19,”alieleza Bi Juma.
Kwingineko, mahakama ya Nyeri Ijumaa ilimhukumu mama aliyepatikana na hatia ya kuuza chang’aa.
Esther Wanjiku alipatikana akiuza chang’aa hapo Ijumaa katika kijiji cha Chaka, eneo la Nyeri.
Kiwete
Akijitetea,
Wanjiku alisema kuwa amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu na anatetemeka kila
wakati kwa athari ya dawa anazokunywa za kupunguza makali ya Ukimwi
(ARVs).
Wanjiku aliomba mahakama pia imsamehe kwani anamlea mtoto kiwete na watoto wengine watatu.
Hakimu mkuu wa Nyeri, Bi Wilbroda Juma alimueleza mshtakiwa kuwa hawezi msamehe bila kuhukumiwa.
“Mahakama imekupata na hatia na utalipa faini ya Sh30,000 au kifungo cha miezi mbili,”alieleza Bi Juma.