Zaidi ya wanafunzi 300 kwa kila kata katika wilaya
ya Mufindi mkoani Iringa, wamebainika kuwa hawajui kusoma, kuandika na
kuhesabu kwa mwaka 2012/2013 idadi ambayo imedaiwa kuongezeka mwaka
hadi mwaka.
Hayo yamebainika katika kikao cha kamati ya ushauri ya Hamashauri ya
Wilaya hiyo, ambapo pamoja na suala la wanafunzi kutojua kusoma kuandika
na kuhesabu pia kikao hicho kimejadili suala la Mimba mashuleni tatizo
ambalo licha ya kupigiwa kelele bado ufumbuzi umekuwa kitendawili.
Wadau wa kikao hicho akiwemo mbunge wa jimbo la Mufindi Kusini
Mendrad Kigola, wametoa maoni mbalimbali kuhusu tatizo la kutojua
kusoma na kuandika, huku upungufu wa vifaa vya kufundishia ukitajwa kuwa
ni sababu mojawapo inayosababisha walimu kushindwa kufundisha kwa
ufanisi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Peter Tweve ametoa
maagizo ya jumla kwa watendaji ili kukabilinana na changamoto ambazo
zimeonekana kukwamisha maendeleo ya sekta ya elimu katika Wilaya hiyo.
Imedaiwa kuwa wazazi wengi, wamekuwa wakimaliza kesi za mimba na
watuhumiwa kwa kishawishi cha fedha na kusababisha kesi hizo
kutofikishwa katika vyombo vya kisheria.