Ajali mbaya yaua, yajeruhi
Vijimambo Blog
Khamisuu Abdalla na Kauthar Abdalla
WATU 21 wamejeruhiwa wengine hali zao zikiwa mbaya na mmoja kufariki
dunia katika ajali mbaya iliyotokea jana asubuhi katika kijiji cha
Mgambo, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Ajali hiyo ililihusisha gari la abiria linalofanya safari zake kati ya
mjini na kijiji cha Mkokotoni na gari ndogo la kutembelea aina ya Noha.
Mashuhuda wa tukio hilo wamesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi,
ambapo gari la abiria lilikuwa likifukuzana na gari jengine linalofanya
safari zake kati ya mjini na Nungwi.
Baada ya kufika katika kijiji hicho dereva wa gari la Mkokotoni
alishindwa kulidhibiti gari lake na kusababisha kugonga Noha na
kupinduka.
Abiria aliefariki ni mtoto alietambuliwa kwa jina la Said Gharib (14)
mkazi wa Gamba ambae alikuwa akisafiri pamoja na baba na mama yake
kwenda mjini kwa ajili ya kutafutiwa nguo za sikukuu, huku hali ya mama
yake ikiwa mbaya.
Miongoni mwa majeruhi hao 12 wametibiwa katika hospitali kuu ya
Mnazimmoja na kuruhusiwa kurejea nyumbani huku tisa wamelazwa katika
hospitali hiyo wakiendelea na matibabu.
Polisi waliosafiri na majeruhi hao walisema, miongoni mwa waliojeruhiwa
ni abiria wawili na dereva wao waliokuwa wakisafiri kwa Noha na dereva
wa gari ya abiria anashikiliwa na polisi kwa mahojiano.
Hiyo ni ajali ya tatu mbaya kutokea katika kipindi cha mfungo wa mwezi
wa Ramadhan, ambapo ajali ya kwanza ilitokea katika eneo la
Mwanakwerekwe wakati gari la jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
lililobeba wanajeshi na raia waliokuwa wakienda kwenye mazishi ya
wanajeshi waliouawa Darfur kupinduka na kujeruhi watu 24.
Ajali ya pili ilitokea Ijumaa, Julai 26 katika barabara ya Maisara baada
ya gari ya abiria inayofanya safari kati ya mjini na uwanja wa ndege
kupinduka na kujeruhi watu 11 na kufanya idadi ya majeruhi wa ajali zote
kufikia 56.