MWANAMUME na mkewe walioingia katika kituo cha polisi bila kujua wakiwa wamelewa kupindukia walishtakiwa katika mahakama ya Kericho.
Walishtakiwa Ijumaa kwa kukosa nidhamu kutokana na ulevi.
Bw David Kiprono Kemei na mkewe Sharon Chepkoech walifikishwa mbele ya hakimu mkuu mwandamizi Kericho Bw Samuel Soita.
Walishtakiwa kutenda kosa hilo mnamo Agosti 1, 2013 katika soko la Kapsoit kaunti ta Kericho.
Kiongozi wa
mashtaka Inspekta Harun Chabari aliambia korti wawili hao waliingia
katika kituo cha polisi wakiwa walevi ndipo wakakamatwa na kushtakiwa.
Hakimu alithibitisha kwamba walikuwa mume na mke alipowauliza ikiwa walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Wawili hao waliomba msamaha wakisema walikuwa na watoto wawili walio na umri wa miaka sita na saba wanaowategemea.
Mahakama iliwasamehe na kuwaonya kwamba wakirudia kosa hilo watachukuliwa hatua kali
Hakimu aliwashauri wapange shughuli za maana za kutenda wanapoenda kutembea.