Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania, TCRA leo imevifungulia vituo vya utangazaji vya
Radio Imaan ya mjini Morogoro na Kwa Neema FM Radio ya jijini Mwanza
vilivyokuwa vimefungiwa kwa miezi sita kutokana na kukiuka Sheria na
Kanuni za Utangazaji.
Uamuzi wa kuvifungia vituo hivyo ulichukuliwa tarehe 26/02/2013 na
Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.
Taarifa hiyo imetolewa leo na TCRA kupitia taarifa kwa vyombo vya habari.
Mnamo tarehe 26/02/2013 Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania ilitoa uamuzi wa kuvifungia vituo vya utangazaji vya Radio
Imaan ya mjini Morogoro na Kwa Neema FM Radio ya jijini Mwanza baada ya
kukiuka Sheria na Kanuni za Utangazaji.
Kamati ya Maudhui iliuita uongozi wa vituo hivyo tarehe 11/02/2013 na
tarehe 14/02/2013 ili kujitetea na vyote vilikiri kosa.
Baada ya
kutafakari utetezi wa Radio Imaan na Radio ya Kwa Neema FM na kwa
kuzingatia Sheria na Kanuni za Utangazaji, Kamati iliamua kutoa adhabu
kwa vituo vyote viliwi kama ifuatavyo:-
a) Vituo vyote vilipewa onyo pamoja na kufungiwa kurusha matangazo kwa
kipindi cha miezi sita kuanzia tarehe 26/02/2013;
b) Vituo vyote vilitakiwa kuithibitishia Mamlaka ya Mawasiliano na
Kamati ya Maudhui kwa maandishi kuwa hawatarejea kutenda kosa la aina
hiyo au linalofanana na hilo. Ikiwa vitarudia Kamati ya Maudhui
haitasita kuvifutia leseni zao za utangazaji.
Kutekeleza adhabu na hatua zilizochukuliwa na vituo hivyo na Mamlaka ya Mawasiliano:
Baada ya Uamuzi huo kusomwa, vituo vyote viwili vilianza kutekeleza
adhabu mara moja kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za
Utangazaji.
Mamlaka ya Mawasiliano ilipokea barua ya udhibitisho wa
kutofanya kosa tena yaani pamoja na sera ya uhariri
(Editorial Policy) na ratiba ya vipindi kutoka kwa vituo vyote viwili.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilifanya ukaguzi kwa vituo vyote viwili
ili kujiridhisha na kuzipitia sera za uhariri pamoja na mwongozo wa
vipindi kabla ya kuvifungulia.
Kurejeshwa kwa Matangazo*
Kamati ya Maudhui iliandika barua tarehe 27/08/2013 kuhusu kuvifungulia
vituo hivyo vya utangazaji vya Radio Imaan ya mjini Morogoro na Kwa
Neema FM Radio ya jijini Mwanza baada ya kutumikia adhabu kwa mujibu wa
Sheria na Kanuni za Utangazaji.
Vituo hivi vimeanza kurusha matangazo
yake kuanzia leo tarehe 28/08/2013 baada ya muda wa adhabu kuisha.
Kamati ya Maudhui inapenda kutumia fursa hii kuvionya vyombo vya habari
vya utangazaji vya redio na televisheni kuwa makini katika kutekeleza
masharti ya leseni pamoja na kufuata Sheria na Kanuni za Utangazaji.
Kamati ya Maudhui haitasita kutoa adhabu kali au kuvifungia vituo
vitakavyokiuka Masharti ya leseni, Sheria pamoja na Kanuni za Utangazaji
au hata kuvifutia leseni zao.
Kamati ya Maudhui inatoa wito kwa vyombo vya habari vya utangazaji
kuzingatia Sheria, Kanuni na Masharti ya leseni ilikuboresha Sekta ya
Utangazaji na kudumisha amani nchini.
Eng. Margaret Munyagi
Mwenyekiti,
Kamati ya Maudhui Ya TCRA,
S.L.P. 474,
DAR ES SALAAM