Bw Sylvester Mwendwa mmoja wa wanaume wawili ambao wamekubali kumuoa mwanamke mmoja wakati wa mahojaino Agosti 25, 2013
MMOJA wa wanaume waliotia saini mkataba kuishi na mwanamke mmoja alitoroka Jumatatu akisema maisha yake yamo hatarini.
Bw Sylvester
Mwendwa, mwenye umri wa miaka 26, alisema aliamua kuacha nyumba zake
mbili ambazo amempangia Bi Joyce Wamboi, baada ya mwanamke huyo kumfokea
kwa kufichua siri ya ndoa hiyo.
Akizungumza na Taifa Leo
kwenye ufuo wa bahari Hindi, alikoenda kupitisha siku akifikiria kwa
kwenda, Bw Mwendwa alisema Bi Wamboi alikasirika sana hasa baada ya
wanawake kumvamia nyumbani kwake mtaa wa Kisimani, Kisauni na kumzoma
wakisema amewaaibisha.
Wanawake hao walisema walikasirishwa na habari katika gazeti la Taifa Leo kwamba Wamboi amejumuisha mwanamume wa pili - Bw Elijah Kimani - katika ndoa yake.
Walimkemea
kwa hasira Wamboi, ambaye alipoteza mumewe kwenye ajali ya barabarani,
kwa kumsaliti Bw Mwendwa, ambaye wanasema wamemtambua kuwa mumewe halisi
kwa miaka yote minne ambayo wamekuwa pamoja.
“Wamekuja
nyumbani na kumkemea mke wangu. Wamemwambia kwamba wamekuwa wakinijua
mimi tu, kumbe yeye amekuwa na mwanamume mwengine ambaye hawamfahamu,”
akasema Bw Mwendwa huku akipangusa machozi.
Alisema bado anampenda Wamboi, ambaye amempangishia nyumba mbili - moja yao wawili na nyingine ya watoto na dada yake Wamboi.
Inasemekana kuwa Bw Mwendwa pia alimfungulia Wamboi biashara ya mboga.
Alisema
biashara hiyo huleta karibu Sh8,000 kwa siku lakini hachukui hata senti
moja ili kumwezesha Wamboi kugharamia mahitaji yake na ya watoto wake
ambao anasema anawachukulia kuwa wanawe pia.
“Nilimpata na
watoto wawili wadogo punde baada ya kufiwa na mumewe. Nilichukua mkopo
benki na kumfungulia biashara. Nimewatunza watoto hao kama wangu bila
kinyongo. Inasikitisha kwamba sasa ameshikana na mwanamume kutoka kwao
na amenikasirikia kwa kutoboa siri,” akasema Bw Mwendwa.
Mmoja wa watoto hao pacha yuko mwaka wa pili katika shule moja ya chekechea.
Bw Mwendwa
pia alipata pigo jingine Jumatatu alipofutwa kazi katika duka la nyama
mjini Mombasa kwa madai kuwa amewaaibisha wanaume kwa ndoa yake hiyo.
Aibu
“Nimefika
kazini leo (Jumatatu) na mwajiri wangu akaniambia sina kazi tena kwa
sababu kitendo nilichofanya ni cha aibu,” akasema.
Na licha ya
kufikwa na mikosi yote hiyo, Bw Mwendwa anasema bado anampenda Bi Wamboi
na kama si kwa hasira alizonazo, yuko tayari kuishi naye wakati wowote.
“Nampenda
sana na sitajali kuwa naye wakati wowote. Nimetoroka tu kwa sababu ana
hasira na yule mwanamume mwengine ni wa kabila lake. Nahofia wanaweza
kula njama waniangamize,” akasema.
CHANZO:TAIFALEO