Wapiga kura wakiwa kwenye foleni mjini Epworth, Zimbabwe Julai 31, 2013. Picha/Habari na AFP
Kura
zinaendelea kuhesabiwa nchini Zimbabwe, baada ya uchaguzi mkuu wenye
ushindani mkubwa uliofanyika mnamo Jumatano. Wapiga kura wengi
walijitokeza kushiriki, huku kukiwa na madai ya njama za wizi wa kura na
wandani wakuu wa rais Robert Mugabe, ili kuendeleza utawala wake wa
miaka 33.
Mpinzani wake
mkuu, Bw Morgan Tsvangirai, alinukuliwa akisema kuwa anatarajia
uchaguzi huo kuwa mwanzo mpya kwa taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Waandalizi
waliripoti kuwa idadi kubwa ya wapiga kura ilijitokeza katika uchaguzi
huo, ulio wa kwanza nchini humo tangu uchaguzi mkuu wa 2008 uliogubikwa
na ghasia, na uliopelekea kubuniwa kwa serikali ya muungano kati ya
viongozi hao wawili.
Hakukuwa na ripoti zozote za uwepo wa ghasia, licha ya kampeni kali zilizojawa na utoaji wa propaganda kati ya wapinzani wakuu.
Katika vituo
vingi, wapiga kura walianza kupiga foleni kabla ya jua kuchomoza, saa
kadha kabla ya kufunguliwa rasmi kwa vituo hivyo.
Upigaji kura uliendelea vizuri, hadi saa za jioni, huku wengine wakilazimika kupiga kura kwa mwangaza wa mishumaa.
Waandalizi walisema kuwa wapiga kura waliokuwa wakingojea katika foleni sharti wangepata nafasi ya kupiga kura zao.
“Watu wote
walio katika foleni wanapaswa kuruhusiwa kupiga kura zao, hata ikiwa
watafanya hivyo saa sita za usiku,” akasema Bi Rita Makarau, mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo.
Rais Mugabe
alipiga kura saa za asubuhi, katika kitongoji kimoja mjini Harare,
alikosema kuwa uchaguzi huo utaendana na matakwa ya wananchi.
“Ninaamini kuwa watu watapiga kura kwa amani na hakuna anayeshurutishwa kufanya uamuzi asioutaka,” akasema rais huyo.
Rais Mugabe alipata umaarufu baada ya kuiongoza nchi hiyo katika harakati za kupigania uhuru kutoka kwa Waingereza.
Haki
Lakini
utawala wake unaoungwa mkono na jeshi umekuwa ukikumbwa na migogoro ya
kiuchumi pamoja na kuhujumiwa kwa haki za kibinadamu, hali ambayo
imepelekea nchio hiyo kutengwa na jamii ya kimataifa pamoja na kuwekewa
vikwazo na mataifa ya Magharibi.
Mnamo Jumanne, Bw Mugabe aliapa kung’atuka mamlakani, ikiwa Bw Tsvangirai angeibuka mshindi.
“Ukishindwa sharti ukubali,” akasema.”Hatujahusika na njama zozote za udanganyifu,” akaongeza rais huyo.
Lakini Bw Tsvangirai, aliye waziri mkuu, alisema kuwa hakikisho hilo litaaminika likitekelezwa.
Bw Tsvangirai
alishinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi mnamo 2008, lakini akadinda
kushiriki katika duru ya pili ya uchaguzi huo, baada ya waungaji wake
mkono 200 kuuawa huku maelfu wakijeruhiwa katika mashambulizi
yaliyoonekana kuungwa mkno na serikali.
Bw Tsvangirai mwenye umri wa miaka 61, amekuwa akishikilia kuwa kuna njama ya kuiba kura katika uchaguzi huo.