JAMII YATAKIWA KUPINGA UNYANYASAJI KWA WATOTO WA KIKE

Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, Mama Salma Kikwete akizungumza katika mkutano wa High Level Group nchini Botswana. Picha na John Lukuwi.

Na Anna Nkinda- Gaborone,  Botswana
JAMII imetakiwa kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa hakuna unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wa kike na kuhakikishwa watoto hao wanalindwa ili wasiingie katika mazingira hatarishi yatakayo wasababishia kupata maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi (VVU).

Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika  katika Hoteli ya Lansmore Masa Square iliyopo mjini Gabarone nchini Botswana.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema huwa anajisikia uchungu pale anaposikia kuwa mtoto wa kike amebakwa au amefanyiwa ukatili wa kijinsia na kuiomba jamii nzima iweze kumsaidia na kumkomboa mwanamke.

“Kama jamii yetu ya nchi za kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika itaungana kwa pamoja na kuamua kumsaidia mtoto wa kike itawezekana kwani hata kama watoto hawa wakipata huduma bora ya afya bila ya kuwapatiwa elimu hakuna jambo la maana watakalolifanya kwakuwa watakuwa na afya bora lakini watakosa kujiamini kwani hawana elimu”, alisema Mama Kikwete.

Akiongelea kuhusu Taasisi ya WAMA alisema kitaaluma yeye ni mwalimu na wakati anafundisha aliona changamoto mbalimbali zinazowakabili watoto wa kike na pale alipoanzisha taasisi hiyo aliamua kuwasaidia watoto wa kike ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi ambao wamekosa nafasi ya kwenda shule ili nao waweze kusoma kama watoto wengine.

Mama Kikwete alisema, “Tuna shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mfano ya WAMA-Nakayama ambayo ina jumla ya wanafunzi 325 wa kidato cha kwanza hadi cha nne pia Taasisi ya WAMA inawagharamia masomo wanafunzi wasichana 300 ambao wanasoma shule mbalimbali za Sekondari katika mikoa yote ya Tanzania.

Alimalizia kwa kuiziomba nchi wanachama wa EAC na SADC kutunga na kufuata sera na sheria zitakazomlinda mtoto wa kike kwa kufanya hivyo ataepukana na unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ubakwaji, udhalilishwaji, kutopewa huduma bora za afya na elimu.

Mkutano huo wa siku mbili uliandaliwa  na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS), UNFPA, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF), Shirika la Chakula Duniani (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lengo kuu likiwa ni kuhakikisha kuwa vijana wote wanapata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia na stadi za maisha jambo ambalo litawasaidia kufahamu zaidi  ugonjwa wa Ukimwi.

Wakati huo huo, Mama Salma amesema bado watoto wa kike wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za udhalilishaji na unyanyasaji wa jinsia, ukosefu wa elimu, utaalamu na huduma zitakazowasaidia kukaa shuleni, kujikinga na mimba za utotoni, ugonjwa wa Ukimwi na virusi vinavyosababisha kansa ya shingo ya kizazi. Mama Salma katoa kauli hiyo wakati akifunga  mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia.

Alisema kwa kufanya kazi kwa pamoja kati ya mashirika yanayofanya kazi chini ya mwamvuli wa Umoja wa Mataifa (UN) na mashirika ya kijamii wanaweza kutambua mahitaji na changamoto zinazowakabili vijana na kuwaomba wakati wanakusanya maoni wawashirikishe viongozi na jamii nzima.

“Tunachotakiwa kufanya kama wanakamati ni kutumia muda tuliopewa kusoma ripoti yote na kuielewa kisha kuwashirika wadau mbalimbali wa wa maendeleo ili waweze kujadili ripoti hii na kutoa maoni yao”, alisema Mama Kikwete.

Naye Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS) Prof. Sheila Tlou alisema miaka ya nyuma Umoja wa Mataifa (UN) ilikuwa inafanya kazi na kila mtu aliyekuwa na mamalaka lakini hivi mashirika yote yaliyopo chini ya UN yanafanya kazi kwa ushirikiano na hivyo kuzisaidia nchi husika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

“Kwangu mimi hii ni historia kwani mpango kazi wa Maputo (Maputo Plan of Action) na makubaliano haya ya leo yatasaidia kushughulikia utolewaji wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kwani jambo hili linatakiwa kuangaliwa kwa umakini zaidi hakika tutafanya kitu katika jamii yetu kwakuwa vijana wanakabiliwa na matatizo mengi ndani ya nchi zetu”, alisema Prof. Tlou.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo