WAKAZI wa eneo la Madogo, kaunti ya Tana River wameonywa wawe macho dhiidi ya watu wanaodaiwa kuuza nyama ya fisi kwa bei rahisi wakiwahadaa raia kwamba ni nyama ya ng’ombe.
Kulingana na chifu wa eneo hilo, Bw
Aaron Kunyo nyama hiyo inaaminika ni ya fisi ambao idadi yao ni kubwa
katika eneo hilo. Alisema wakaguzi wa nyama wamekuwa wakikosa kugundua
nyama hiyo ambayo sasa inauzwa kwa bei nafuu ya Sh40 kwa kilo moja
ikilinganishwa na nyama halisi ya ng’ombe ambayo bei yake ni Sh120 kwa
kilo.
“Imekuwa ikiuzwa vichochoroni hasa
kuanzia saa kumi na moja asubuhi hadi saa saba mchana. Wauzaji wamekuwa
wakiificha katika mabandali ya unga,” alisema Bw Kunyo.
Chifu huyo ilisema msako wa dharura
uliofanywa na afisi yake na wakazi ulipelekea kukamatwa kwa mtu mmoja
ambaye alikuwa akiuza nyama inayoaminika kuwa ya fisi.
Mtu huyo ambaye alikamatwa akiwa na kilo 90 za nyama alipatikana na ngozi ya mnyama huyo wa mwitu.
“Tumepeleka sampuli za nyama hiyo
kwa maabara ya serikali na punde tu baada ya matokeo kutolewa, mwanamume
huyo atafunguliwa mashtaka,” alisema Bw Kunyo.
Ripoti hizo zimezusha hofu miongoni
mwa wakazi wa eneo hilo ambao wengi wao ni waislamu. Kulingana na
tamaduni za wakazi wa eneo hilo, mtu akila nyama za mnyama yeyote wa
mwituni hupata laana na mifugo wake wanaweza kufa wote.
Mzee Juma Bagana, mkazi wa eneo
hilo, alisema shida hiyo imesababishwa na ukosefu wa kichinjio katika
eneo hilo. Alisema wauzaji nyama na wenye hoteli hutengemea kichinjio
cha mjini Garissa.
Matapeli
“Serikali ya kaunti ya Tana River
inapaswa kuharakisha mipango ya kujenga kichinjio hapa Madogo ili
kuwakinga wakazi dhidi ya matapeli wanaowahadaa. Hilo likifanywa,
tutaweza kuwachinja wanyama wetu hapa, nyama ikaguliwe na tununue nyama
iliyothibitishwa kuwa salama,” alisema Mzee Bagana.
Tukio hili limeibua kumbukumbu
katika nchi jirani ya Somalia ambako wanamgambo wa Al Shabaab walianza
kuwauzia nyama ya fisi watu wa maeneo waliyoyadhibiti ili kuchangisha
pesa za kufadhili shughuli zao.
Kulingana na kundi hilo, nyama ya fisi hutumiwa kwa kuvunja laana na pia kuwaepusha watu dhidi ya magonjwa.
Hata hivyo, viongozi wa dini ya
kiislamu kwa muda mrefu wamesisitiza msimamo wa kuwakataza waumini wao
dhidi ya kula nyama ya fisi hsa ikizingatiwa kwamba mnyama huyo hula
mizoga ya wanyama wengine na pia binadamu.