Wake
wa viongozi Jumuiya ya Uamsho Zanzibar, wameiomba serikali kuitazama
kesi inayowakabili viongozi hao kwa jicho la uadilifu, haki na sheria
ili kuonesha dhana ya utawala bora.
Wakizungumza
na waandishi wa habari katika kongamano la wanawake wa Kiislamu
lililofanyika msikiti wa Mbuyuni, kinamama hao wamelalamikia kesi hiyo
kuchukua muda mrefu huku ikiwa hakuna hatua yoyote muhimu inayochukuliwa
ili haki itendeke.
Wametaka
vyombo vya sheria vifanye kazi kwa maadili, hasa ikizingatiwa kwamba
Zanzibar ni mshiriki wa Muungano wa Tanzania ambayo ni mwanachama wa
taasisi mbalimbali za kulinda na kuheshimu haki za binadamu ulimwenguni.
“Hatukusudii
kuingilia kazi za mahakama, bali tunaeleza hali halisi ya uvunjwaji wa
sheria na katiba ya nchi kwa vyombo vya sheria kufanya kazi kwa utashi
bila ya kuzingatia haki za wanachi mbele ya sheria”, walidai wanawake
hao.
Walidai kuwa, kitendo cha kunyima haki kinaweza kuitia doa kubwa mahakama na serikali mbele ya macho ya kimataifa.
Aidha,
walitaja sababu za kuwekwa ndani waume zao kuwa ni harakati zakuongoza
umma wa Wazanzibar kudai haki yao ya msingi juu ya hatima ya Zanzibar
kuwa nchi yenye uhuru wa kujiamulia mambo yake.
Wameeleza
kusikitishwa kwao kwa kusema kuwekwa ndani kwa waangalizi hao wa
familia zao, kumewaathiri sana kisaikolojia na kiuchumi.
Pia
wamesema mwenendo mzima wa taaluma za Kiislamu ambazo viongozi hao
walikuwa wakifundisha katika madarsa mbalimbali kwenye misikitini na
vyuo, umeathiriwa na kushikiliwa kwa viongozi hao.
Kwa
hivyo wamevitaka vyombo vya sheria kufanya haki katika maamuzi yao ili
kudumisha amani na utulivu uliopo pasi na kutia dosari serikali ya umoja
wa kitaifa iliyowalea Wazanzibari pamoja.
Kupitia
kongamano hilo, wanawake hao wameviomba vyombo vya sheria, kuwaruhusu
viongozi hao kuonana na wake na ndugu zao wakati wanapofikishwa
mahakamani kwa kusikilizwa kesi yao.
Katika
hatua nyengine, kinamama hao wameunda kamati ya kufuatilia na kuratibu
mwenendo wa kesi pamoja na kuonana na watendaji wa haki za binadamu.