MEYA ILEMELA ATISHIA KUMUUA MBUNGE

1736 
MEYA wa Manispaa ya Ilemela, Henry Matata, amefunguliwa jalada polisi akidaiwa kutishia kumuua mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (CHADEMA), katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemema, Amina Masenza.

Matata ambaye ni Diwani wa Kata ya Kitangiri aliyevuliwa uanachama wa CHADEMA mwaka jana kutokana na kusababisha mgogoro ndani ya chama mkoani Mwanza lakini alifungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo ambapo kesi hiyo bado inaendelea.

Hata hivyo katika hatua ya kushangaza, Septemba mwaka jana, Matata alichaguliwa kwenye mkutano ambao ulikuwa haukidhi akidi ya wajumbe ambao ni madiwani 14 na kwa mujibu wa sheria ndio wanaounda halmashauri hiyo mpya iliyomegwa kutoka katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini hapa, Kiwia alisema Matata alimtishia kumuua Julai 26, mwaka huu, katika kikao hicho na kwamba tayari amefungua jalada polisi mkoa Mwanza kulalamikia vitisho hivyo.

Kiwia alisema kuwa chanzo cha vitisho hivyo ni msimamo wake wa kumpinga Meya Matata kuongoza kikao hicho ambapo siku hiyo mbunge huyo alisimama na kumuomba Mkurugenzi wa Manispaa, Zuberi Mbyana, amteue mwenyekiti wa muda ili aongoze kikao.

Alisema kuwa alifikia uamuzi huo kutokana na madiwani wa CHADEMA kutomtambua Matata kama Meya wa Manispaa hiyo wakilalamikia uchaguzi uliomweka madarakani kuwa ulikuwa batili kwa vile alichaguliwa na madiwani sita wa CCM na CUF bila kuwepo madiwani wao nane.

“Siku ya kikao niliomba ateuliwe mwenyekiti wa muda aongoze kikao maana Matata si Meya wa Ilemela kisheria. Baada ya kusema hivyo, Matata alisimama na kusema angeliniua. Alirudia kauli yake mara mbili tena mbele ya mkuu wa wilaya, polisi na wajumbe wengine waliohudhuria kikao hicho,” alisema.

Kiwia alidai kushangazwa na kitendo cha mkuu wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya pamoja na askari waliokuwepo kikaoni kunyamazia tukio hilo na kushindwa kumkamata Matata na kumchukulia hatua.

Alisema kuwa kwa sasa ana mashaka na usalama wa maisha yake kwani kitendo cha mkuu wa wilaya kushindwa kumchukulia hatua meya huyo kinatia hofu juu ya usimamizi wa sheria.

“Kwa kweli nashindwa kuelewa utendaji wa mkuu huyu wa wilaya, yaani mtu anasimama mbele yake na kumtishia mtu maisha halafu yeye na askari wanakaa kimya tu,” alihoji.

Kiwia aliongeza kuwa baada ya vitisho hivyo, yeye pamoja na madiwani wenzake wawili wa CHADEMA, Rosemary Brown wa Kata ya Pasiansi na Gradis Kiwia wa viti maalumu walitoka nje ya kikao huku Matata akitishia kumfukuza udiwani Brown.

Alipoulizwa jana kuhusu tuhuma hizo za kutishia kumuua Kiwia, Matata alisema mbunge huyo asiogope kuuawa maana asipomuua yeye atauawa na wengine endapo hatapunguza mdomo.

Katika hatua nyingine, meya huyo anadaiwa kushikiliwa kwa muda na Jeshi la Polisi Wilaya ya Ilemela juzi kwa tuhuma za uchochezi.

Matata anadaiwa kuwahamasisha wananchi wa Mhonze kuwapiga mawe maofisa wa jiji la Mwanza watakapokwenda eneo hilo kugawa viwanja.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, polisi ilimshikilia kwa mahojiano zaidi kuhusu tuhuma hizo za uchochezi. Matata alikiri kuwaamuru wananchi wa kijiji cha Mhonze kuwafanya hivyo lakini alikanusha kuhojiwa na polisi badala yake alisema alikwenda kituoni kwa masuala mengine na si vinginevyo.

“Kweli niliwaapia wawapige mawe watu wa jiji maana watakwendaje kupima na kugawa viwanja eneo lisilo lao.”
Uchaguzi wa Matata ulikiuka kanuni na sheria za halmashauri. Kwa mujibu wa sheria ni kwamba akidi ya wajumbe iliyokuwa ikihitajika kwa ajili ya meya kupigiwa kura ni madiwani tisa badala ya madiwani sita walioshiriki kwenye uchaguzi huo.

Badala yake Matata alichaguliwa kuwa meya na madiwani sita pekee, wanne wa CCM na mmoja wa CUF baada ya madiwani wengine wa CHADEMA kususia mkutano huo wa uchaguzi.

Matata alichaguliwa wakati suala lake la kufukuzwa uanachama ndani ya CHADEMA likiwa bado linangojea uamuzi wa mahakama alikofungua kesi kupinga uamuzi wa chama chake.

 source Tanzania Daima


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo