Kamanda
mpya wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP.Geofrey Kamwela akitoa
taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya matukio
manne ya mauaji likiwemo la mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi
Mariamu Alphonce (9) kuuawa na kaka yake Elibariki kwa kukatwa katwa
kwa panga na kutenganishwa mwili na kichwa.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Jeshi
la polisi mkoa wa Singida limefanikiwa kumkamata Elibariki Alphoce (21)
mkazi wa kijiji cha Kizega wilaya ya Iramba, anayetuhumiwa kumuua mdogo
wake Mariam (9) mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi
Kizega.
Elibariki anatuhumiwa kumuua mdogo wake Mariam Julai 16 mwaka huu katika kijiji cha Kizega.
Inaelezwa
kuwa Elibariki alimkata kata kwa mapanga mdogo wake sehemu mbalimbali
za mwili na kisha kuteganisha kichwa na kiwiliwili.
Habari za uhakika kutoka kijijini hapo zinadai kuwa Elibariki ni mtumiaji sugu wa madawa ya kulevya aina ya bhangi.
Kamanda
wa jeshi la polisi mkoa wa Singida ACP Geofrey Kamwela, amesema
mtuhumiwa huyo amekamatwa Julai 18 mwaka huu akiwa amejificha kando
kando ya mto Ruruma wa kijiji cha Ruruma tarafa ya Kiomboi.
Katika
tukio jingine, Kamanda Kamwela amesema katika msako mkali unaoendelea
mkoani Singida, wanawake wanne wamekamatwa wakimiliki pombe haramu aina
ya gongo lita 93 na mtambo moja wa kutengenezea pombe hiyo ambayo ni
hatari kwa afya ya viumbe hai.
Amewataja
watuhumiwa hao na lita za gongo kwenye mabano kuwa ni Khadija Ikaku
(63) mtambo ya kutengeneza (gongo) na Rehema Idd mwenye umri wa miaka 30
(lita 10), wote wakazi wa kijiji cha Makiungu wilaya ya Ikungi.
Kamwela
ametaja wengine kuwa ni Grace Naftali (22) mkazi wa kijiji cha Makingu
wilaya ya Ikungi (lita tano) na Neema Mwaja (42) mkazi wa kata ya
Majengo Manyoni mjini (lita 12).