Rais wa Tanzania Jakaya Kiwete amewaongoza maelfu ya
waombolezaji katika kutoa heshima zao za mwisho kwa wanajeshi saba wa
Tanzania waliouawa nchini Sudan.
Saba hao walikuwa katika harakati za kulinda
amani chini ya Muungano wa Afrika katika jimbo la Darfur nchini Sudan
tarehe 13 mwezi Julai.
Miili ya wanajeshi hao iliwasili mjini Dar es
Salaam siku ya Jumamosi, na kupokelewa na mamia ya waombolezaji
walioongozwa na makamu wa rais Dokta Gharib Bilal, katika uwanja wa
kimataifa wa ndege wa Julius Nyerere kabla ya kupelekwa katika chumba
cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya kijeshi ya Lugalo.
Hafla ya kuwaaga wanajeshi hao inaendelea katika uwanja wa makao makuu ya jeshi eneo la Upanga.
Rais Kikwete anawaongoza jamaa familia na rafiki wa wanajeshi hao kuwapa heshima zao za mwisho kabla ya maziko nyumbani kwao.
Wanajeshi hao wa TPDF ni pamoja na Sajenti
Shaibu Shehe, Corporal Oswald Chaulo, Corporal Mohammed Ally, Corporal
Mohammed Chukilizo, Private Rodney Ndunguru, Private Fortunatus Msofe na
Private Peter Werema.
Rais wa Sudan Omar Al Bashir wiki jana
alimhakikishia rais Jakaya Kikwete kuwa wote waliohusika katika
kuwashambulia wanajeshi hao na kuwaua watakamatwa na kuchukuliwa hatua
za kisheria.
Rais Bashir alitoa ahadi hiyo wakati wa
mazungumzo na Kikwete akiongeza kuwa anaamini waliohusika na mauaji hayo
walikuwa wahalifu na kuwa lazima wasakwe.