Habari zilizotufikia hivi punde vurugu zimezuka maeneo ya Ubungo jijini Dar es salaam (karibu na Tanesco) jioni hii kati ya Askari Polisi, Mgambo wa jiji na wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu wamachinga.
Kutokana na vurugu hizo, zaidi ya askari mgambo 33 wa Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na jeshi la Polisi wametumia nguvu kuwaondoa wafanya biashara ndogo ndogo waliopo katika eneo la Ubungo na kusababisha kuzuka kwa vurugu hizo.
Watu walioshudia vurugu hizo wamesema kwamba operasheni hiyo imefanyika kwa kushtukiza saa 12:00 jioni ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuwaondoa machinga hao kutoka eneo hilo ambalo linapakana na ukuta wa Tanesco na kituo cha mabasi Ubungo.
Mmoja wa wafanyabiashara ndogo ndogo, Hamisi Hassan Mwinyimkuu amesema kwamba hawezi kuhama katika eneo hilo kwa kuwa kuna soko zuri la kuuzia bidhaa zao.
"Hatuwezi kuhama hapa, tufanyabiashara katika eneo lenye wateja wengi. Lakini tunaomba kama inawezekana serikali ikakutana na sisi ili kujadili suala hili," amesema Mwinyimkuu.
chanzo:habarimasai.com