Rais
Barack Obama wa Marekani amemteua mshirika wake wa muda mrefu Susan
Rice kuwa mshauri wake mkuu wa masuala ya usalama, nafasi ambayo
haihitaji kuthibitishwa na baraza la Seneti.
Wakati
akiwa katika nafasi yake ya zamani kama Balozi wa Marekani katika Umoja
wa Mataifa, Rice aliingia matatani kuhusiana na maelezo yaliyotolewa na
utawala juu ya shambulizi dhidi ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini
Benghazi Libya, mwaka uliyopita.
Wapinzani wa chama cha Republican walimtuhumu Rice kwa kutoa taarifa za upotoshaji zenye lengo la kuficha ukweli.
Rais
Obama amemsifu Rice kama mtumishi wa umma aliekamilika, mzalendo ambae
hutanguliza nchi yake, jasiri na anaye elewa kuwa hakuna mbadala kwa
uongozi wa Marekani.
Obama pia amemteua Samantha Power, mtaalamu wa haki za binaadamu, kuwa balozi mpya katika Umoja wa Mataifa.
Uteuzi wa Samantha Power lazima uthibitishwe na baraza la Seneti.