Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-Moon ameikosoa sheria mpya iliyopitishwa na serikali ya Burundi, ambayo amesema itaathiri uhuru wa vyombo vya habari. 

Mapema wiki hii Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi  aliiridhia sheria hiyo, ambayo imekosolewa na mashirika ya habari na yale ya haki za binaadamu.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Martin Nesirky, amesema Katibu Mkuu Bw. Ban Ki-Moon amesikitishwa na sheria hiyo, yenye vifungu vinavyoweza kukandamiza uhuru wa habari, huku akisisitiza kuwa haki ya uhuru ya kujieleza na sekta huru ya habari ni mambo muhimu kwa ustawi wa demokrasia.

Sheria hiyo iliyopitishwa na bunge la Burundi mwezi April, inadhoofisha ulinzi wa vyanzo vya habari, inadhibiti kuripoti habari za uchunguzi na inawataka waandishi wote kuwa na shahada ya Chuo Kikuu bila kujali uzoefu. 

Pia inapiga marufuku kusambaza taarifa au nyaraka kuhusu mada za ulinzi au taarifa zinazochukuliwa kuwa propaganda za adui, au zinazoweza kuathiri uchumi wa Burundi.