ASKARI MLEVI ATIA AIBU MKESHA WA MWENGE

Na Eliya Mbonea, Karatu
ASKARI polisi mwenye cheo cha koplo, amegeuka kituko baada ya kuwasili katika mkesha wa Mwenge katika viwanja vya Mazingira Bora wilayani Karatu, huku akiwa amelewa. Mlinzi huyo wa amani aliyekuwa amevaa nguo za kiraia, alionekana akiwa anajivinjari katika viwanja hivyo kama raia wa kawaida, huku akiyumba kutokana na kuzidiwa kilevi.

Huku taratibu nyingine zikiendelea, ghafla askari waliokuwa kazini uwanjani hapo walimvuta pembeni ya gari la polisi na kumuamuru aondoke haraka eneo hilo.


Kituko zaidi ni pale askari huyo alipolazimika kutoa heshima kwa wakubwa zake, alijikuta akijilazimisha kukakamaa kama sehemu ya kutoa heshima.

Hata hivyo, kituko zaidi kilichotolewa na askari huyo baada ya kuondolewa zilipita takriban dakika 15 kisha alirejea tena akiwa amevalia nguo zake za FFU na viatu vya kazi.

Kwa mara nyingine tena askari waliokuwa uwanjani hapo wakiongozwa na bosi wao walionekana tena wakimshikilia na kumvuta pembeni kimya kimya na kumuonya kwa kitendo alichofanya.

Mwandishi wa habari hii akiwa eneo la tukio alishuhudia askari huyo akiamuriwa kupanda gari namba DFP 750, Landrover kisha maagizo yalitolewa kwa askari mmoja kuwa aende akalale mahali husika.

Kuondoka kwa askari huyo uwanjani hapo, kulitoa nafasi kwa wananchi wa Karatu waliokuwa wamefurika kwenye viwanja vya Mazingira Bora, kuburudika na kucheza muziki usiku kucha.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo