VIJANA WAUNGANA KUTOA HUDUMA YA UMEME KATA YA LUDENDE WILAYANI LUDEWA

Hizi ndizo nguzo zinazosambaza umeme katika kijiji cha Ludende
Bw.Nicky Komba msambazaji nishati ya umeme kijiji cha Ludende
Bw.Agustino Msigwa msambazaji umeme katika kijiji cha Ludende
wajumbe wa serikali ya kijiji wakitoka katika mkutano wa kujadili namna huduma hiyo inavyotolewa
   
Na Nickson Mahundi
Vijana watatu katika kijiji cha Ludende kata ya Ludende wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe wameungana kwa pamoja ili kuweza kuboresha huduma ya umeme waliyokuwa wakiitoa katika kijiji cha Ludende.
 

Vijana hao ambao walianza kutoa huduma hiyo mwaka 2009 wakiwa tofauti kwa kila mmoja kuzalisha umeme wake na kusambaza katika mtaa ambao yeye anaishi ambapo waliweza kuzifikia nyumba 69 wameamua kwa dhati kuungana na kusambambaza umeme huo katika kata nzima ya Ludende.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Bw.Agustino Msigwa ambaye ni mmoja wa vijana hao alisema kuwa huduma hiyo ilianza kutolewa mwaka 2009 kupitia mto Vombwe lakini yeye pekeyake aliweza kusambaza umeme huo katika nyumba 21.

Bw.Msigwa alisema wao hawajasomea masuala ya umeme lakini kupitia vipaji walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu waliweza kufanya ubunifu ambao uliwasaidia kufikia malengo yao ya kuzalisha nishati ya umeme ikiwa kila mmoja alizalisha katika eneo lake.

“mimi na wenzangu ambao ni Bw.Nicky Komba na Francis Mwinuka kila mmoja kwa muda wake tumeweza kutoa huduma hiyo lakini tunapata wasiwasi baada ya kutokea watu wengine kutueleza tuache kuyatumia maji ya mto huo eti kwakua hatujafuata hatua za kisheria baada ya kupata habari kuwa tumeungana ili tuweze kusambaza kata nzima”,alisema Bw.Msigwa.

Naye Bw.Nicky Komba mmoja wa vijana hao alilaani kitendo cha watu wasiojulikana kuuingilia mto huo kwa kuwataka wasitishe huduma yao kwa kua hawana elimu ya kutosha kukutana na mamlaka husika.

Bw.Komba alisema wao wameshafikia hatua nzuri katika umeme wao na wamekubaliana kuungana ili kuipanua huduma hiyo lakini hawana utaalamu wa kutosha hivyo wanaziomba mamlaka husika na wafadhiri mbalimbali kuwasaidia ili kufikisha huduma hiyo kwa wananchi wengi zaidi.

Alisema wamepata taarifa kuwa tayari kuna watu wameshaulipia mto huo katika mamlaka ya bonde la ziwa Nyasa na REA ambapo wao hawazijui ofisi za mamlaka hizo kutokana na kutokuwa na uelewa wakutosha hivyo wanawaomba watanzania wanaozijua ofisi hizo ili waweze kuiendeleza huduma hiyo.

Aidha mmoja wa wananchi wa kijiji cha Ludende Bw.Vasco Msigwa alikili kuwepo umuhimu wa huduma inayotolewa na vijana hao kwani ni miaka mine mpaka sasa huduma ya umeme inapatikana katika kijiji chao bila matatizo yoyote.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo