UKOSEFU WA MAJI WAKARIBISHA HATARI SHULE YA MSINGI NDULAMO WILAYANI MAKETE

Mwalimu mkuu Godigodi Malangalila
Shule ya msingi Ndulamo iliyopo kijiji cha Ndulamo wilayani Makete ipo hatarini kukumbwa na magonjwa ya milipuko kama kipindupindu na kuhara kutokana na ukosefu wa maji, hali inayowalazimu wanafunzi kujisaidia kwenye vyoo vya shule hiyo bila maji

Akizungumza na mtandao huu ofisini kwake mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw. Godogodi Bosco Malangalila amesema tatizo hilo limekuwa sugu shuleni hapo hivyo linahatarisha usalama wa wanafunzi na wakati mwingine hadi waalimu

Amesema tatizo hilo linahatarisha afya za wanafunzi wake kwani pamoja na ukosefu huo wa maji wakati mwingine shule hulazimika kuvunja vipindi na kuwaagiza wanafunzi kwenda kuchota maji kwenye mito ama visima ambayo si safi na salama kwa matumizi ya binadamu lakini wao hulazimika kuyatumia hivyo hivyo


“Ndugu mwandishi inasikitisha kwa kweli, hapa shuleni huwa tunatoa uji kwa wanafunzi lakini maji hata ya kuosha vyombo hakuna, ya kutumia vyooni nayo hakuna na vyoo vya shule ni vile vya kutumia maji, lakini wanafunzi huenda kujisaidia hivyo hivyo bila maji” alisema Mwalimu Malangalila

Ameongeza kuwa mara nyingi vyoo hivyo huziba na kulazimika waalimu wenyewe kuvizibua vyoo hivyo na wakati wengine kuwaita wazazi kuja kuzibua vyoo hivyo lakini hivi sasa wazazi wengi hugoma kuja kufanya shughuli hiyo kwa madai kuwa wao wanachanga fedha za maji kijijini hivyo ni jukumu la vyombo husika kufikisha maji shuleni hapo ili kuinusuru shule hiyo

nyumba iliyoshindwa kukamilika kwa wakati
“Tangu nimefika hapa shuleni kama mwalimu mkuu mwezi Julai 2012, nimeshafunga shule kwa tatizo hili hili, kwa kuwa tunazidiwa” alisema 

Katika hatua nyingine mwalimu huyo amesema tatizo hilo la ukosefu wa maji pia limeathiri ujenzi wa nyumba ya mwalimu shuleni hapo ambapo ujenzi huo ulikuwa ukamilike Oktoba mwaka jana lakini hadi hivi sasa nyumba hiyo imefikia sehemu ya linta, na tatizo kubwa ni ukosefu wa maji

Tamali Sanga
Kwa upande wake Tamali Cyprian Sanga anayesoma darasa la saba shuleni hapo ambaye pia ni dada mkuu wa shule hiyo amesema tatizo hilo linawathiri kwa kiasi kikubwa kwani inawallazimu kuosha vyombo vya chakula kwa kutumia maji ambayo si safi na salama na pia wanakosa vipindi na kwenda kuchota maji mtoni ama kwenye visima ambavyo vipo mbali na shule

Amesema kuwa vyoo wanavyovitumia kwa hivi sasa ni vichafu na hakuna maji ya kuvifanyia usafi na pia wanalazimika kuvitumia hivyo hivyo

Kaka mkuu wa shule hiyo Alexanda Marko amesema wakati mwingine kutokana na uchafu uliokithiri kwenye vyoo hivyo wanafunzi wengine wanalazimika kurudi makwao kujisaidia huku wengine wakijisaidia kwenye msitu wa shule hiyo ambao uko jirani na vyoo hivyo hivyo kuwataka wahusika kulishughulikia ipasavyo tatizo hilo 

Shule ya Msingi Ndulamo ina jumla ya wanafunzi 633 ambao wanategemea maji ili kuendesha shughuli mbalimbali katika shule hiyo

NB:- PICHA ZA VYOO HIVYO NIMESHINDWA KUZIWEKA KWA SABABU YA KIMAADILI


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo