Na Waandishi Wetu
MAGHOROFA yaliyojengwa kandokando ya Mto Mlalakua na Ufukweni mwa Bahari ya Hindi yatabomolewa, hivyo kuzua mshtuko mkubwa kwa wamiliki.
MAGHOROFA yaliyojengwa kandokando ya Mto Mlalakua na Ufukweni mwa Bahari ya Hindi yatabomolewa, hivyo kuzua mshtuko mkubwa kwa wamiliki.
Uchunguzi
uliofanywa kwa zaidi ya wiki nne umebaini kwamba kazi ya
kubomoa nyumba hizo inaweza kuanza wakati wowote ingawa kuna changamoto
kubwa kwani baadhi ya nyumba hizo ni za vigogo wenye madaraka makubwa
serikalini au ndani ya vyama vya siasa.
Vyanzo
vyetu vya habari vinadai kwamba baadhi ya nyumba hizo zina hati
zilizopatikana serikalini wakati zingine wamiliki wao walivamia maeneo
hayo na kuporomosha maghorofa makubwa.
Kutokana na ujenzi huo holela, wakazi wa Kawe kwa Malecela waliamua kumwandikia barua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wakitoa malalamiko juu ya ujenzi huo.
Barua hiyo ambayo iliyoandikwa Februari 20, mwaka huu ilieleza kwamba ujenzi wa nyumba hizo umekuwa ni kero kubwa kwani zimejengwa katika mkondo wa maji hivyo mvua inaponyesha inasababisha mafuriko kwa wananchi wengine.
Wananchi
hao wamemueleza waziri kwamba nyumba hizo zimeziba mkondo wa maji
katika baadhi ya mito inayoingia baharini, hivyo kusababisha maji kuhama
na kuelekea kwenye nyumba zao na daraja la eneo la Malecela kusombwa na
maji hivyo kusababisha magari kutopita.
Walidai kuwa nyumba nyingi zimejengwa katikati ya mto na wengine wamejaza vifusi kando ya mto unaopita karibu na nyumba zao, hivyo kusababisha mkondo wa maji kwenda kwa wananchi.
“Hivi
sasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanashindwa kutembelea ufukwe wa
bahari kutokana na baadhi ya nyumba kuziba njia na mbaya zaidi
waliojenga kando ya mkondo wameharibu mikoko,” imesema sehemu ya barua
hiyo.
Waliendelea kusema kwamba vigogo hao ambao ni wavamizi baadhi yao wamekuwa wakitembea na bastola hadharani na kuwatishia maisha wale wanaodiriki kuzungumzia ujenzi wanaoufanya katika maeneo hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Hifadhi ya Mazingira nchini (NEMC), Ignas Mchallo alisema:
“Wote waliojenga katika maeneo hayo watahamishwa kwa kufuata sheria kwani kuna wengine waliojenga kabla ya sheria ya mazingira ambayo inataka kuwepo kwa nafasi ya mita 60 toka mtoni au ufukweli,” alisema Mchallo.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka alisema kwamba nyumba 73 zilizojengwa kwenye fukwe za Bahari
ya Hindi, zitavunjwa na akazitaja kuwa ziko kwenye fukwe za Kawe, Mbezi
na Msasani na kwamba ingawa zilijengwa kihalali baada ya kupewa hati,
lakini sheria mpya hairuhusu nyumba hizo kuwepo.
Habari hii imeandikwa na Makongoro Oging’ Haruni Sanchawa na Issa Mnally wa Global Publishers.