Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema ipo haja kwa Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kufikiria upya
uamuzi wake wa kutengua usajili wa Katiba ya TFF ya mwaka 2012 na kutaka
itumike ya mwaka 2006, kwani hautekelezeki.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo mchana, mara baada ya kikao cha Kamati ya
Utendaji, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema ni muhimu jambo hilo
likaangaliwa upya kwa sababu athari zake ni mbaya, na pengine Dk.
Mukangara hakushauriwa vizuri kabla ya kufanya uamuzi huo.
“Kamati ya
Utendaji ya TFF haitaki kubishana na Mheshimiwa Waziri hata kidogo, ila
tunaamini wakati anatamka haya hakufahamu madhara yake, athari zake na
ugumu wa utekelezaji wake. Kwa waliomshauri hili, wamemshauri vibaya,”
amesema Rais Tenga.
Amesema rai ya
TFF kwa Waziri ni kuwaita ili wamweleze ni kitu gani wafanye kunusuru
mpira wa miguu wa Tanzania, kwani wanaamini jambo hili litakwisha baada
ya kumwelimisha hasa kutokana na ukweli kuwa kabla ya kufanya uamuzi huo
hakuwasikiliza.
Katika mkutano
huo, Rais Tenga alianza kwa kusema kuwa TFF inaiheshimu sana Serikali,
hivyo inaheshimu maagizo yaliyotolewa na Waziri, lakini akaongeza kuwa
TFF ina wajibu wa kutoa ufafanuzi juu ya maagizo hayo.
Amesema lengo
la kuelezea historia ya TFF ilikotoka ni kubaini migongano ya maagizo
hayo na taratibu za TFF ambazo kwa bahati mbaya zinasigana na maagizo
hayo.
Rais Tenga
amesema TFF ni chombo cha wanachama, ambapo wanachama wake ni vyama vya
mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu, na ina taratibu za kufanya
uamuzi kwa mujibu wa Katiba yake na za wanachama wake ambazo
zimeidhinishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema si TFF
pekee, bali vyama vya nchi zote ambavyo vimeunganishwa na Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), zinaheshimu na kufuata maagizo na
miongozi ya shirikisho hilo la kimataifa la mpira wa miguu.
Rais Tenga
amesema TFF haitakiwi kuingiliwa katika uongozi na uendeshaji wake,
kwani jambo hilo likitokea rungu la FIFA litaiangukia TFF, na madhara
yake ni makubwa. Miongozo ya FIFA inasisitiza uhuru wa wanachama wake
katika uendeshaji shughuli za mpira wa miguu, na iko kwenye Katiba ya
TFF.
“Sheria za
nchi ndizo zilizozaa Katiba ya TFF. TFF ni chama kamili kinatakiwa
kufanya uamuzi wake ili mradi uzingatie madhumuni ya kuanzishwa kwake.
Leo TFF ikiacha mpira wa miguu na kuanza kujishughulisha na gofu, hapo
Msajili ana haki ya kuingilia,” amesema Rais Tenga.
Kuhusu maagizo
ya Waziri, Rais Tenga amesema kifungu cha 11 cha Sheria ya Baraza la
Michezo la Taifa (BMT) kinazungumzia usajili wa chama, na si marekebisho
ya katiba, ingawa kanuni zinahusu marekebisho ambapo ameongeza kuwa
uamuzi wa marekebisho ni wa Mkutano Mkuu na si Msajili.
“Ukienda
kuomba viza, fomu unapewa na yule anayekupa viza. TFF tulipowasilisha
marekebisho ya Katiba hatukupewa fomu. Msajili akasema sawa. Jambo la
kujaza fomu si la TFF, ndiyo maana tunasema ipo haja ya jambo hili
kufikiriwa upya.
“Usajili
tayari umepita, kwamba Msajili hakutoa fomu, mwathirika anakuwaje TFF?
Tunaona ni muhimu jambo hili likaangaliwa upya,” amesema Rais Tenga na
kuongeza kuwa utaratibu wa kusajili Katiba ya 2006 ambayo ndiyo Waziri
ameagiza itumike ulikuwa huo huo uliosajili Katiba ya 2012.
Akizungumzia
historia ya TFF kutoka mikononi mwa BMT, Rais Tenga amesema ni zao za
Katiba ya 2004 ambayo ilifanyiwa marekebisho ukumbini na kugongwa mhuri
na Msajili hapo hapo na kuingia kwenye uchaguzi. Katiba hiyo ndiyo
iliyoiondoa BMT kuisimamia TFF.
“Huko ndiko
tulikotoka, si kwa kulazimishwa, bali kwa kupewa Katiba ya 2004. Katiba
ina utaratibu mzima wa kufanya uamuzi. Maelekezo ya Waziri yamesahau
huko tulikotoka siku nyingi. Uhalali wa marekebisho unatokana na ridhaa
ya Mkutano Mkuu. Hiyo ni kwa mujibu wa Katiba yenyewe, hakuna nafasi ya
BMT,” amesema.
Amesema katika
maagizo ya Waziri, ameitaka TFF kufuata Katiba ya 2006 na kanuni za
BMT, lakini Katiba hiyo hiyo ya 2006 haina nafasi ya BMT, na hata kama
TFF ingetaka kutekeleza hilo haliwezekani.
“Kwa maagizo
haya inaonekana Waziri kashauriwa vibaya. Tunajua hakuwepo katika nafasi
hiyo (2004) wakati wa makubaliano kati ya Serikali na FIFA kuacha mpira
wa miguu ujiendeshe wenyewe,” amesema Rais Tenga.
Pia
amezungumzia umuhimu wa Katiba toleo la 2012, kwani kuna marekebisho
mengi yalifanyika mwaka 2007, 2008, 2009 na 2011 ambapo ukiyafuta maana
yake unakiweka pembeni Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), Bodi ya
Wadhamini, wanachama wapya (mikoa), Bodi ya Ligi, Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi, Leseni za Klabu na Kanuni za Fedha.
“Kwa uamuzi
huu yote yaliyofanyika hayana maana. Waziri sidhani kama alikuwa
anafahamu athari za maagizo yake. Kama angelijua asingefanya uamuzi huo.
Si rahisi kurudi katika Katiba ya 2006. Hao wajumbe wa Katiba ya 2006
unawapata wapi? Maana yake hata vyama wanachama ni batili kwa vile
vimerekebisha Katiba zao 2009 na 2010,” amesema Rais Tenga.
Amesema kwa
Serikali kufuta, maana yake ni kutengua uamuzi wa TFF ambapo madhara
yake ni nchi kufungiwa, ambapo timu za Taifa hazitacheza mpira, klabu
hazitashiriki michuano ya kimataifa na wadhamini nao watakaa pembeni kwa
vile hawawezi kudhamini timu ambazo hazishindani kimataifa.
“Dhana kwamba
tukae tu tusicheze nje, ni dhana ya watu walio nje ya mpira wa miguu.
Dhamira yetu ni kuhakikisha hatufungiwi. Waziri ametuagiza tupeleke
barua FIFA kuwa ametengua marekebisho ya katiba. Hatupeleki hivyo, kwani
hiyo ni Government interference, watatufungia.
“Nia yetu bado
ni Waziri kutupa nafasi ya kutusikiliza,” amesema Rais Tenga na
kuongeza kuwa kuhusu uchaguzi kwa vile FIFA wanakuja ombi la TFF kwa
Waziri ni kuacha kwanza mchakato uendelee hadi ufike mwisho.
“FIFA
wanakuja, tuwasubiri. Nilidhani utaratibu huo utaheshimika. Kama mtu wa
mpira haitaki FIFA anataka nini? Ahadi yetu ni kuhakikisha watu wanapewa
haki. Hiyo ndiyo ahadi yetu na tumeisimamia, na ndiyo maana FIFA
wanakuja,” amesema.
Akijibu swali
kuhusu waraka, Rais Tenga amesema marekebisho ya Katiba hayakufanywa kwa
siri, ridhaa ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kufanya marekebisho hayo kwa
njia ya waraka ilipatikana ambapo 70 waliunga mkono na 33 walikataa.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
