Mwongozo kuhusu Muundo, Utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya
Katiba ya Wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake
uliotangazwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba haujazingatia maoni ya
msingi yaliyotolewa na wadau mbalimbali ikiwemo Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA).
CHADEMA inawatahadharisha wananchi kuhusu ‘mianya ya uchakachuaji’
iliyotolewa na muongozo huo kwa kuzingatia kuwa ‘uchakachuaji’ wa uteuzi
wa wajumbe wa mabaraza ya katiba, ni ‘uchakachuaji’ wa utoaji maoni
kwenye mabaraza ya katiba, ambayo ni hatua ya awali ya ‘uchakachuaji’ wa
rasimu ya katiba.
Kwa mujibu wa Muongozo huo, ‘mianya ya uchakachuaji’ imeachwa kwenye
ngazi ya kamati ya maendeleo ya kata ambayo wajumbe wake ni madiwani na
wenyeviti wa mitaa/vijiji ambao kwa mujibu wa matokeo ya chaguzi za
mwaka 2009 na 2010 kuna hodhi kwenye vikao hivyo ya chama kimoja
(CCM).
Lakini bila kuzingatia hali hiyo, Tume ya Mabadiliko ya katiba kupitia
muongozo huo imewapa mamlaka ya kuchagua wajumbe wa mabaraza ya katiba
katika kila kata kwa upande wa Tanzania Bara.
Muongozo huo ‘umeminya’ mamlaka ya wananchi wote kupitia mikutano yao ya
vijiji na mitaa kwa upande wa Tanzania Bara kuwa ni ‘kupendekeza’ tu
majina badala ya kuchagua.
Hata hivyo, muongozo huo umetangaza utaratibu tofauti kwa upande wa
Zanzibar ambapo wawakilishi wakishaguliwa na wananchi kwenye mkutano wa
Shehia majina yao yanawasilishwa moja kwa moja bila kuwa na ‘mianya ya
uchakachuaji’ kama ilivyo kwa Tanzania Bara.
Hivyo, pamoja na kuwahimiza wananchi wakiwemo wanawake na vijana kuomba
kwenye ngazi ya kijiji na mitaa kuwa wajumbe kwenye mabaraza hayo ya
katiba; CHADEMA inawahimiza pia wananchi na wadau kudai kwamba mara
baada ya wananchi kuchagua wawakilishi wao kupitia mikutano mikuu maalum
kwenye vijiji na mitaa, wawakilishi hao waingie moja kwa moja kwenye
mabaraza ya katiba bila kuchujwa na vikao vinavyotawaliwa na CCM.
Itakumbukwa kwamba tarehe 14 Februari 2013, CHADEMA kiliwasilisha kwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba maoni na mapendekezo ya CHADEMA juu ya
muongozo uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu muundo,
utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya (Mamlaka
za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake.
Maoni na mapendekezo yaliyowasilishwa katika nyaraka ya kurasa tisa
yalihusu vipengele vyote kumi vya rasimu ya muongozo iliyotolewa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba.
Katika maoni na mapendekezo hayo, CHADEMA pamoja na mambo mengine
hakikubaliana na muundo wa kuwa mabaraza hayo ya wilaya yatakuwa na
wawakilishi walioteuliwa na ngazi ya kata; badala yake CHADEMA
kilipendekeza kuwa wajumbe wote waliochaguliwa kuwakilisha vijiji au
mitaa au shehia waingie moja kwa moja kwenye mabaraza ya wilaya.
Ikumbukwe kuwa upungufu katika mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya
wananchi binafsi ilisababisha idadi ndogo ya watu waliotoa maoni ambapo
mpaka awamu nne zinakamilika jumla ya watu 318,223 tu ndio waliotoa
maoni sawa na asilimia 0.7 ya wananchi wote zaidi ya milioni 44.9.
CHADEMA kilieleza kuwa muundo na utaratibu huu ni muhimu katika kujenga
muafaka wa kitaifa na katika kurekebisha upungufu katika mchakato
uliotangazwa kukamiilika wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi binafsi
uliofanyika kwa awamu nne mwaka 2012 ambapo tume ilifanya mikutano 1776
tu na wananchi wachache kutoa maoni kutokana na sababu mbalimbali.
Imetolewa tarehe 1 Machi 2013 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
