MAMA AMTUPA MTOTO PORINI WILAYANI LUDEWA

Wilaya ya Ludewa
Na Nickson Mahundi
Mtoto wa jinsi ya kiume amenusurika kifo wilayani Ludewa katika mkoa wa Njombe baada ya kuzaliwa na kutupwa porini na mama yake jirani na makazi ya watu na kuokotwa na raia wema ambapo walimuwahisha hospitali ili kuokoa maisha yake.

Akiongea na waandishi wa habari Muuguzi wa zamu katika hospitali ya wilaya ya Ludewa Bi.Eda Muhema alisema alimpokea mtoto huyo kutoka kwa wasamaria wema waliotokea Ludewa Kijijini mtaa wa songambele majira ya jioni Februari 28 mwaka huu akiwa katika hali nzuri kutokana na wasamaria hao kumsitiri kwa nguo nzito.

Bi.Muhema alisema mtoto huyo aliletwa akiwa na uzito wa kilo tatu na akiwa ameshakatwa kitovu kwa kutumia panga hivyo alichokifanya yeye ni kukipunguza kitovu hicho na kumtengeneza kitaalamu zaidi.

“tumempokea akiwa salama kama mnavyomuona lakini inaonekana amezaliwa usiku na kapigwa na baridi lakini kutokana na umahiri wa akinamama waliomuokota waliweza kumpa huduma ya kwanza na kufunika nguo nzito ili kumsaidia kurudisha joto lake la mwili,”alisema Bi.Muhema.

Kwa mujibu wa shuhuda mmoja wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Mrs.Kidulile ambaye ni muuguzi mstaafu alisema ilikuwa ni majira ya jioni februari 28 mwaka huu aliona wanafunzi wakishangaa kitu katika shamba la mahindi.

Ndipo alipowauliza kunani hapo nao wakamjibu kuwa kuna kitoto kichanga kimetupwa hapa alisema kutokana na taaluma yake alifika eneo la tukio na kubaini kuwa mtoto huyo alikuwa bado yuko hai,akawaita wanawake wenzie na kuchukua nguo ili kumfunika.

Mrs.Kidulile alisema mtoto huyo alitupwa jirani na makazi ya watu ambapo palikuwa na maji yakitiririka kutoka katika bomba lililo pasuka lakini maji hayo hayakuweza kumfikia alipolazwa.

Alisema walimkuta mtoto huyo akiwa hajakatwa kitovu na akiwa kaviringishwa katika gunia hivyo walilazimika kumkata kitovu kwa kutumia panga alilobeba mama mmoja aliyekuwa akienda shambani na kumuwahisha hospitali ili ahifadhiwe vizuri.

 Katika kuulizia kwa wajirani ndipo walipompata mwanamke aliyemtupa huyo mtoto wakamchukua na kumfikisha katika kituo hicho cha polisi cha Ludewa mjini ambako mwnamke huyo anaendelea kushikiliwa na jeshi la Polisi.

Aidha mama huyo Bi.Magdarena Lugongo anayetuhumiwa kwa kosa la kumzaa mtoto na kumtupa akihojiwa na waandishi wa habari alikiri kutenda kosa hilo na kueleza sababu kubwa ni ugomvi ndani ya ndoa.

Bi.Magdalena alisema alifanya uamuzi huo kutokana na hasira kwani mume wake aliye mtaja kwa jina la Andrea Kayombo aliukataa ujauzito huo kuwa sio wake na kumpa manyanyaso makubwa pindi ana ujauzito.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo