Jelard Lucas, Mwanza
AMA kweli pombe mwanaharamu, ukimkuta mtu anasifia pombe basi mpe
pole yake kwani hayo ni matumizi mabaya ya akili alizopewa bure na
Mwenyezi Mungu, hali imejidhihirisha kwa mkazi mmoja wa Kwimba, Mwanza,
Nhende Ng’wanandilima (35) aliyeliwa na fisi sehemu kubwa ya uso wake.
Tukio
hilo lilitokea katika Kijiji cha Kibetelwa maeneo ya Nh’ungumalwa,
Kwimba ambapo imeelezwa kuwa Nhende alikumbana na kisanga hicho baada ya
kunywa ulabu kupita kiasi hivyo kulewa chakari, hali iliyomsababishia
kushindwa kujitambua na kuanguka kwenye pori la kijiji hicho na fisi
kumkuta.
Kwa mujibu wa mashuhuda, wakati kijana huyo akiliwa, alipiga kelele
zilizofika kwenye kijiji hicho ambapo majirani walifika na kumnusuru
kisha kukimbiza Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa Nhende, hali aliyonayo kwa sasa inamnyima raha kwani
amekuwa kilema, kitu ambacho hakufikiria kinaweza kutokea maishani
mwake.
Hata hivyo, alieleza kuwa daktari mashuhuri wa masuala ya koo na
mfumo wote wa ‘ogani’ za fahamu amempa matumaini baada ya kumuahidi
kumtengeneza upya sehemu zote zilizoliwa na fisi huyo.
“Hali hii si nzuri kwani napata maumivu makali, sikuwahi kujua kama
fisi anaweza kumla binadamu hivi, pia namshukuru Mungu nimekatwa nyama
za mapaja Jumatatu ya wiki hii ili kusukwa upya kwa mfumo wote wa sura
yangu, Dokta Gliyoma ndiyo mkombozi wa maisha yangu.
“Nawashauri vijana wenzangu waache pombe kwani ina madhara makubwa kama niliyoyapata mimi,” alisema.