
Watoto Yatima waliohudhuria katika sherehe za maadhimisho
ya siku ya Mtoto Yatima,wakiwa katika Ukumbi wa Salama Bwawani Mjini
Zanzibar,zilipofanyika sherehe hizo,kwa ushirikiano wa jumuiya ya
Muzdalifa na shirika la misaada la I.H.H la Nchini Uturuki Jana na
kuhudhuriwa na wananchi na Viongozi mbalimbali.
----------
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesema kuwa Serikali itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha
inafikia hatua nzuri katika kutoa huduma kwa jamii hasa watoto
mayatima huku akisisitiza haja ya kuwalea katika maisha bora na yenye
furaha.
Dk.
Shein aliyasema hayo jana katika sherehe ya siku ya mtoto yatima,
zilizofanyika katika ukumbi wa Salama Bwawani mjini Zanzibar na
kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais
Maalim Seif Sharif Hamad, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar
Kabih, Balozi wa Uturuki Mhe. Ali Daud Gul,wazee, wazazi pamoja na
watoto yatima kutoka ndani na nje ya Zanzibar.
Dk.
Shein alisema kuwa azma ya Serikali ni kujenga misingi imara kwa jamii
ya watoto na watu wazima ili kuwajengea wananchi maisha bora zaidi.
Alisema
kuwa hatua za kusaidia watoto yatima zinakwenda sambamba na juhudi za
serikali ya Mapinduzi Zanzibar tokea kuasisiwa na Marehemu Mzee Abeid
Amani Karume alipofungua nyumba ya watoto yatima Forodhani mara tu baada
ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
Aliongeza
kuwa katika kuendeleza huduma hiyo, Serikali ikishirikiana na Taasisi
ya ZAYEDESA imewahamisha watoto yatima kwenda nyumba ya kisasa Mazizini
na inatoa ushiriki mkubwa na Taasisi ya SOS katika kuendeleza kijiji cha
watoto yatima Mombasa Unguja ambapo ipo skuli ya msingi na Sekondari
pamoja na kupitisha Sheria Namba 6 ya mwaka 2011 yenye lengo la
kuhakikisha haki za watoto, ulizni na ustawi wao.
Katika
hotuba yake hiyo Dk. Shein alisema kuwa misaada na shughuli zao ni
kuipunguzia mzigo Serikali ambayo hutumia kiasi kikubwa cha fedha katika
uimarishaji wa sekta hizo hapa Zanzibar.
Dk.
Shein aliwanasihi wazazi kuunga mkono juhudi za Jumuiya ya Muzdalifa
kwa kuwekeza katika kuwalea vyema watoto yatima ambao mara nyingi
wanakuwa nyuma.
Alieleza
kuwa wazazi na walezi wanawajibu mkubwa kwa watoto yatima kwa kuwapa
elimu, chakula kizuri, kuwapenda na kuwakinga na unyanyasaji, hasa wa
kijinsia jambo ambalo litapelekea kuwa na vijana madhubuti walio na afya
njema, elimu na uzalendo
“Suala la malezi mema kwa watoto yatima ni la lazima kwani wasemavyo wahenga’usipoziba ufa utajenga ukuta”,alisema Dk. Shein.
Aidha,
Dk. Shein alieleza kuwa kuvunjika kwa amani ni miongoni mwa mazingira
yanayosababishwa na binaadamu na kupelekea kuwepo kwa watoto yatima
wengi.
Alisema
kuwa dunia imekuwa ikishuhudia hali ilibvyokuwa mbaya katika baadhi ya
nchi, Mashariki ya Kati, Asia na hata eneo la Afrika ambapo maelfu ya
watoto wamebakia yatima kutokana na kukosa amani.
Alisisitiza
kuwa hali hiyo inabainisha umhyimu wa kutunza amani na usalama kwani
bila ya amani ni mtafaruku wa jamii na kuhatarisha maisha ya watoto.
Pamoja
na hayo, Dk. Shein alitoa nasaha kwa jamii kujali na kudumisha amani
miongoni mwa jamii pamoja na kujikinga na maradhi thakili na hatari ya
ukimwi kwani ni maradhi yanayosababisha vifo vya wazazi na hatimae
kuwaacha watoto yatima.
Dk.
Shein alieleza haja ya kuzingatia hali iliyojitokeza nchini hivi sasa ya
kuwepo watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambapo wengine hukosa
mahala pa kula, kulala, hawapati elimu na kwa jumla wanakuwa hawana
mwelekeo mwema wa maisha yao.
“Ni
wajibu wetu tushirikiane ili tuweze kuwaondoshea hali hii watoto
wetu…naipongeza Wizara ya Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Vijana, Wanawake
na Watoto kwa jitihada zao ni vyema taasisi nyengine zikashiriki katika
kuliondoa tatizo hili ambalo lipo mijini”,aliongeza Dk. Shein.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein aliitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuwa
karibu na Jumuiya ya Muzdalifah na kutoa shukurani kwa Jumuiya zote za
ndani na nje ya Zanzibar zikiwemo I.H.H ya Uturuki, WEFA ya Ujerumani na
Al-ANSAR FOUNDATION ya Uiengereza kwa kutoa michango yao mikubwa ya
kuiunga mkono Jumuiya ya Muzdalifah ili iweze kufaya kazi zake vizuri.
Nae
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Abubakar Khamis, alieleza kuwa Serikali
imekuwa ikishirikiana na taasisi mbali mbali katika kuhakikisha watoto
yatima wanapata huduma zinazostahiki ili waweze kuishi vizuri.
Nae
Mbunge Mstaafu wa Bunge la Uturuki Mhe. Husnu Tuna akitoa salamu zake
kutoka kwa Jumuiya ya I.H.H alisema kuwa tatsisi hiyo imekuwa ikitoa
misaada ya kibinadamu ambayo lengo lake ni kuondoa matatizo ya watoto
mayatima ambapo imekuwa ikiiunga mkono Tanzania kwa mwaka wan ne hivi
sasa na inalea mayatima 29,000 katika nchi 41.
Aidha,
katika risala yao Jumuiya ya Muzdalifah ilieleza kuwa imekuwa ikitoa
huduma mbali mbali zikiwemo huduma za kuwasaidia watoto yatima, huduma
afya, maskulini, madrasat, zakka, sadaka, maafa, kuchimba visima na
huduma nyenginezo.
Nao
watoto yatima walieleza furaha zao kwa mgeni rasmi kwa kuungana nao
katika siku yao hiyo adhimu na kutoa ombi lao la kuitaka siku hii iwe ya
Kitaifa.