Waamini wakiwa kanisani wakati wa Misa Takatifu |
Iringa
ASKOFU Jimbo Katoliki la Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumta amesema damu ya watanzania inayomwagika juu ya ardhi ya, wahusika wa matukio hayo wataulizwa na Kristo aliyejitoa sadaka kwa ajili ya ukombozi.
ASKOFU Jimbo Katoliki la Iringa Mhashamu Tarcisius Ngalalekumta amesema damu ya watanzania inayomwagika juu ya ardhi ya, wahusika wa matukio hayo wataulizwa na Kristo aliyejitoa sadaka kwa ajili ya ukombozi.
Gustav Chahe mwandishi wa mtandao huu anaripoti kuwa Mhashamu Ngalalekumtwa ameyasema hayo leo wakati wa maadhimisho ya Misa Takatifu ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Kiaskofu Parokia ya Kihesa jimboni humo.
Askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania alisema kuwa inatia shaka kwa wahusika wa matukio hayo kuwa huenda wakawa si watanzania ambao wamejaliwa upendo na ushirikiano pamoja na kuheshimiana.
Amesema wapo baadhi ya watu wanaowafanya wenzao kuishi kama wakimbizi jambo ambalo ni kinyume na mpango wa Mungu aliyesema watu wote waishi kwa ushirikiano na upendo kwa kusaidiana katika kudumisha amani ya mtu binafsi na ya taifa kwa ujumla.
“Tuendelee kuwa wanyonge? Hii ni balaa! Hii ni nchi yetu lakini kwa nini wengine wawe kama hawana haki?” amehoji askofu Ngalalekumtwa.
Hata hivyo alisema wenye dhamana ya kulinda usalama na kuruhusu mambo haya kutendeka hakuna haja ya kuendelea katika nafasi hizo kwa sababu wameshindwa kuwajibika kutimiza haki za watanzania.
“Tuliombee Taifa letu. Na hao wenye dhama ya kulinda usalama wa taifa hili na kuzembea hawana haja ya kuendelea kuongoza nafasi zao kwa sababu wameshindwa. Njia yao hao ni motoni tu kwa sababu kazi ya Kristo ni kudumisha amani na upendo” amesema.
Amesema binadamu ana akili fupi, finyu na ndogo ambayo anahitaji msaada wa Kristo aliyejitoa kwa ajili ya kuwakomboa wanadamu ili apate nguvu na kuongezewa ufahamu wa mambo.
“Binadamu ana kila aina ya dhuruma, ana kila aina ya ufidhuli na ana kila aina ya manyanyaso lakini Kristo pekee ndiye anayetaka tuwe wapole na watu wenye kujitathimini na kuomba msamaha na msaada kwake” amesema.
Amesema kiongozi anayependa kutumia mabavu katika kazi na maamuzi yake hana tofauti na viongozi waliomsulibisha Yesu msalabani.
“Ukiona unatafuta sababu ya kugombana na Kristo ujuwe una shida kichwani na mwisho wake ni mbaya. Kiongozi asiyetambua hayo ni mfidhuli na fisadi” amesema.