WANAFUNZI wa Shule ya Msingi ya Dk. Omari Juma, wamemtaka Mwanasheria wa Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam kumaliza mgogoro wa gereji bubu zinazozunguka shule hiyo.
Wakizungumza na waandishi wa
habari katika eneo la shule hiyo, wanafunzi hao walisema kama kero yao
haitasikilizwa haraka, kinyume chake wataandamana hadi kwa mkurugenzi wa
manispaa hiyo.
Walisema uwepo wa gereji hizo
ukichanganyika na uvunjifu wa maadili kwa kuwasumbua watoto wa kike,
kumekuwa kukishusha taaluma ya wanafunzi wa shule hiyo.
Mmoja wa wanafunzi hao, Ever
Joseph, alisema wamekuwa wakishindwa kuzingatia masomo kutokana na
makelele ya vyuma wakati wa matengenezo ya magari.
Naye Yusufu Saidi, alisema
wanasikitishwa na mafundi hao kutumia lugha za matusi wakati wanaporuka
ukuta kwa ajili ya kwenda kujisaidia katika choo cha shule hiyo.
Alisema wakati mwingine inatokea
magari yanasababisha ajali kwa kugonga ukuta wa shule hiyo, kitendo
kinachotishia maisha ya wanafunzi hao.
“Mazingira haya yanachafuliwa
hovyo, kama mnavyoona shule yetu yote imezunguukwa na gereji, mafundi
seremala na mafundi nguo ambao wote hao wamekuwa wakijiingiza katika
vitendo vya udanganyifu wa kimapenzi kwa dada zetu na kuwapotosha
kielimu,” alisikitika Saidi.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,
Triphonia Kahwili, aliomba serikali kuingilia kati mgogoro huo ili kila
mmoja kati ya shule hiyo na wamiliki wa gereji kufanya kazi zao kwa
kufuata sheria