Tarehe 19 Februari 2013 Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alifanya ziara ya
kikazi katika kata za Kimara na Saranga kufuatilia kuhusu matengenezo ya
barabara na daraja la Golani.
Mnyika alifanya hivyo siku mbili tangu afanye mkutano wa kikazi na
viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Kanuni na wananchi katika kata ya Mabibo
tarehe 16 Februari 2013 kulitolewa malalamiko kuhusu Kampuni ya Maji
Safi na Maji Taka (DAWASCO) kutoshughulikia maombi ya wananchi
yaliyowasilishwa kwa kampuni hiyo kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka
2010 mpaka 2012.
Ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji huo kuhusu barabara, Mnyika alikutana na
wananchi ambapo walipaswa kulipwa fidia inayokadiriwa kufikia shilingi
milioni 278 ili kuruhusu njia mbadala kupatikana kufuatia ujenzi wa
daraja katika eneo hilo.
Aidha, Mbunge amekagua matumizi ya daraja hilo yaliyoanza kupitia njia
ya zamani na athari zake katika mfumo mzima wa usafiri katika eneo
husika; na kubaini kwamba daraja husika haliwezi kuzinduliwa pamoja na
kuwa limeanza kukamilika mpaka ujenzi wa kingo za mito ukamilike pamoja
na kupatikana kwa barabara mbadala baada ya wananchi kulipwa fidia.
Mara baada ya ziara hiyo Mbunge alikutana na uongozi wa Manispaa ya
Kinondoni na kuwasilisha madai hayo ya wananchi ambao miezi zaidi ya
sita imepita toka nyumba zao ziwekewe X bila hata ya kufanyiwa tathmini.
Baada ya Mnyika kuwawakilisha wananchi hao uongozi wa Manispaa umeamua
kutuma timu ya uthamini na mara baada ya uthamini huo, kutuma uongozi
kukamilisha majadiliano na wananchi husika kabla ya tarehe 25 Februari 2013.
Itakumbukwa kwamba tarehe 6 Mei 2011 Mbunge Mnyika alitembelea kata za
Saranga na Kimara kufuatilia utekelezaji wa mipango ya maendeleo na
kuwajulisha wananchi wa maeneo husika kwamba jumla ya shilingi milioni
zaidi ya mia tano (501,973,470) zilitengwa kwenye bajeti ya Halmashauri
ya Kinondoni kwa mwaka wa Fedha 2011/2012 kwa ajili ya kujenga Daraja
Kubwa la Burura/Golani katika Mto Ubungo.
Baada ya ujenzi wa daraja hilo kuchelewa mbunge alichukua hatua za
kufuatilia kwa mara nyingine mwezi Aprili 2012 na hatimaye mkataba wa
ujenzi wa daraja husika umesainiwa kati ya Manispaa ya Kinondoni na
Mkandarasi Kika Co. Ltd kwa gharama za shilingi milioni 447. Gharama za
ujenzi huo zimeongezwa kwa nyakati mbalimbali mpaka kufikia milioni 672.
Ifahamike kwamba kutokuwepo kwa daraja katika eneo hilo miaka mingi
kulifanya mawasiliano katika maeneo hayo kuwa magumu nyakati za mvua na
kusababisha madhara ya kibinadamu na mali wananchi wanapovuka mto katika
eneo hilo wakati wa mafuriko.
Baada ya mbunge kuwawakilisha wananchi kwa kushirikiana na madiwani
kutaka ujenzi wa daraja hilo, liliingizwa kwenye bajeti ya Manispaa ya
Kinondoni kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kwa vyanzo vya ndani (own
source).
Imetolewa tarehe 20 Februari 2013 na:
Aziz Himbuka
Katibu Msaidizi
Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Ubungo