Nitafuatilia ahadi alizotoa Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe tarehe
17 Februari 2013 kuwa maji yataanza kutoka kata ya Goba tarehe 20
Februari 2013 na ziara ya Mkuu wa Wilaya Jordan Rugimbana kwenye kata
hiyo.
Hata hivyo, ni vizuri umma ukatambua kuwa pamoja na mabadiliko ya hoja
kwa kuongeza maneno ya kupendekeza hoja kuondolewa yaliyofanywa na
Waziri wa Maji Prof. Jumanne Maghembe kinyume na kanuni za Bunge tarehe 4
Februari 2013, maelezo na hoja binafsi niliyowasilisha bungeni
yameongeza uwajibikaji wa Waziri wa Maji, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni na
Halmashauri kuhusu masuala ya maji.
Siku chache baada ya kutangaza tarehe 10 Februari 2013 kwenye mkutano wa
hadhara kuipa Serikali wiki mbili, Mkuu wa Wilaya na Meya wa
Halmashauri ya Kinondoni waliitisha mkutano na viongozi wa mitaa pamoja
na kamati za miradi ya maji ya jumuiya na leo tarehe 18 Februari 2013
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana ameanza ziara ya
ufuatiliaji wa miradi ya maji katika Jimbo la Ubungo.