Picha na maktaba
Na Denis Mlowe, Iringa
HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa imefanikiwa kuingiza kiasi
cha shilingi milioni 10 kwa muda wa wiki chache tangu kuanza kwa kufanya kazi
kwa Greda la halmashauri hiyo walilopata mkopo kutoka Benki ya CRDB
Hayo yalizungumzwa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa
ya Iringa Amani Mwamwindi wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake na kusema kwamba katika mradi huo wamejiwekea malengo kwa mwaka kuweza
kuingiza kiasi cha shilingi milioni 50 ila kwa kuwa malengo hayo yameanza
kuonekana kwa muda mfupi sana hivyo lengo linaweza kuzidi kiwango kwa mwaka.
“mradi wa greda uko chini ya kamati uliyoundwa na baraza la
madiwani na kwa muda wa wiki chache wadau watatu wamejitokeza na kuweza kukodi
greda hili na kuweza kuingiza kiasi hicho cha pesa ambacho inaleta matumaini kwamba
hatukosea kukopa toka benki ya CRDB” alisema Meya Mwamwindi
Wakati huo huo Kikao cha Kamati ya Uongozi wa baraza la Madiwani
wameridhia ombi maalumu toka kwa wafanyabiashara wa Soko Kuu la Iringa la
kutaka kufanya biashara kutoka saa 12 asubuhi hadi saa 2 usiku kutokana na
ungezeko na ukuaji wa kasi wa mkoa wa Iringa na watu wengi kutaka huduma hiyo
iongezwe muda.
Mwamwindi alisema kwamba kutokana na hilo jukumu la ulinzi
wa mali zao litakuwa ni wafanyabiashara wenyewe na kazi ya halmashauri
itaongeza taa katika soko hilo licha ya kuwa na taa baadhi ya sehemu.
Mfanyabiashara wa nyanya sokoni hapo Hussein Juma amepokea
kwa furaha sana suala hilo na kusema kwamba kwa sasa hata vipato vyao
vitaongezeka na amelishukuru baraza la
madiwani kwa kuweza kuridhia ombi lao.
“Hakika kwa wametenda haki na hasa kwa sisi wafanyabiashara
wadogo kwani mji wa Iringa unaongezeka kwa kasi hivyo watu wanahitaji huduma
kwa muda wote kama ilivyo baadhi ya mikoa hapa Tanzania kwani kuna baadhi ya
wafanyakazi wanachelewa sana kurudi hivyo iko safi sana” alisema Juma