Zaidi ya wanachama
70 wa chama cha chadema wa kijiji cha Loiborsoit Kata ya Ngage
Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara wamekihama chama hicho na kujiunga na CCM
baada ya kuona maendeleo yanayofanyika kwenye wilaya hiyo.
Tukio hilo
limetokea wakati katibu mwenezi wa CCM wa Wilaya ya Simanjiro Sumleck Ole
Sendeka wakati akiongea na wananchi wa kijiji cha Nadonjuka ambapo
alieleza kuwa wanachama hao wamerudisha kadi hizo wiki iliyopita
kijijini kwao Loiborsoit.
Alisema kuwa pamoja na wanachama hao pia Katibu kata wa Ngage wa chama
hicho bwana Kiula naye alirudisha kadi ya Chadema na katibu kata ya Orkesumet
Mangajii naye alirudisha kadi ya Chadema na kujiunga na CCM.
Katibu huyo Mwenezi wa wilaya ambaye pia ni Diwani wa kata ya
Naberera alisema wanachama hao wamejiunga na CCM baada ya kurudisha kadi za
Chadema kutokana na kujionea maendeleo yaliyofanyika kwenye wilaya hiyo.
Alisema
wanachama hao waliona siyo vizuri kuwa kwenye upinzani ili hali maendeleo
yamefanyika ikiwemo ujenzi wa barabara za vijijini zilizopo wilayani humo na
upatikanaji wa huduma za afya kwenye zahanati na vituo vya afya.
“Pia wanalima mazao yao kwa kutumia ujenzi wa mifereji ya
umwagiliaji na huduma za elimu zimeboreshwa kuanzia shule za msingi hadi
sekondari na visima vya maji vimechimbwa sehemu mbalimbali,” alisema Ole
Sendeka.
Kwa upande
wake,Katibu wa CCM wa wilaya hiyo,Jamilah Mujungu alieleza kuwa lengo la ziara
yao ni kuwatembelea wanachama wao ili kubaini na kuzishughulikia kero na
changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Katika ziara
hiyo waliweza kutembelea vijiji na kata mbalimbali ili kuangalia
utekelezaji wa ilani ya CCM inavyofanyika kwani wananchi walikuwa na imani
kubwa na chama hicho hadi wakakichagua ili kiwaongoze.
