WATU saba wamefariki dunia na wengine zaidi ya 40
kujeruhiwa kufuatia mabasi mawili kugongana uso kwa uso katika Kijiji
cha Nyatwali Wilayani Bunda Mkoani Mara.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake, Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Mara Kamishina Msaidizi, Absalom Mwakyoma alisema ajali hiyo
ilitokea majira ya saa 11 jioni ikihusisha mabasi mawili ya Mwanza
Coach lenye namba za usajili T 756 AWT aina ya scania marcopolo mali ya
Halfan Ahmed wa mwanza likitoka Musoma kuelekea Mwanza pamoja na basi la
Bestline lenye namba T 535 AJR lililokuwa likitokea Mwanza kuelekea
Sirari.
Mwakyoma alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa mabasi
hayo na madereva kutokuwa makini ambapo yalifika katika eneo la barabara
ambayo inafanyiwa ukarabati na kupita kwa mwendo kasi.
“Madereva wa mabasi yote mawili walikuwa katika mwendo kasi katika
barabara ya vumbi inayofanyiwa ukarabati na hawakuweza kuonana na
kusababisha kugongana uso kwa uso na kupelekea vifo vya watu saba na
zaidi ya 40 kujeruhiwa.
“Watu sita walifariki palepele katika eneo la ajali na mtu mmoja
alifariki muda mchache baada ya kufikishwa katika Hospitali teule ya
Wilaya ya Bunda DDH,” alisema kamanda Mwakyoma.
Kamanda Mwakyoma alisema majeruhi wa ajali hiyo wamelezwa katika
Hospitali ya DDH na kati yao wanne kati 14 ambao walikuwa hawajitambui
wamepelekwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi
kwani hali zao sio nzuri kutokana na kuvuja damu nyingi na hivyo
hospitali ya wilaya ya bunda kutokidhi mahitaji ya damu.
Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi
maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda na kuwaomba Wananchi kwenda
kuitambua.
“Madereva wote wawili wamekimbia mara baada ya kutokea kwa ajali hiyo
lakini kila siku tumeendelea kuwahelimisha madereva juu ya mwendo kasi
lakini bado wapo madereva wasiokuwa makini na tutaendelea kuwachukulia
hatua kali wale wote wana kaidi.
“Lakini abiria nao inabidi wasaidie katika hili wanapoona madereva
wanakwenda mwendo kasi mara wamzue na mara waonapo askari wa usalama
barabarani watoe taarifa,”alisema Mwakyoma.
Baadhi ya abiria walikuwemo kwenye mabasi hayo walisema kuwa mabasi
hayo yalikuwa na mwendo mkali ambapo walijaribu kupiga kelele kuwaambia
madereva kupunguza mwendo lakini hawakuweza kusikilizwa na muda mfupi
ajali ikatokea.
Walisema kuwa ni vema sasa Serikali ikachukua hatua kali kwa madereva
wazembe ili kuzinusuru roho za watu ambao ni nguvu kazi ya taifa ambazo
zinateketezwa kwa uzembe wa madereva.
Hii inakuwa nia ajali ya pili ya mabasi ya abilia kutokea katika
barabara ya Musoma kwenda Mwanza ndani ya wiki mbili baada ya kutokea
ajali nyingine ya basi la Bunda Express likitopkea Wilayani Bunda
kuelekea Mtukula.
CHANZO: www.shommibinda.blogspot.com