MTANDAO WA JINSIA TANZANIA WATOA MAONI YA KATIBA MPYA


TGNP bango linaloonesha ofisi za TGNP

Mapendekezo ya TGNP Katika Maoni ya Katiba Mpya
1. Utangulizi
1. 0 UTANGULIZI
1.1 SHUKRANI
 Mheshimiwa Jaji Warioba -Mwenyekiti Tume ya Katiba
 Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani – Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Katiba
 Wajumbe wote wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba

Mtandao wa Jinsia Tanzania unapenda kutoa shukrani za dhati kwa Tume ya Katiba kwa kutupa nafasi ya kipekee kutoa maoni yetu katika mchakato huu. Kwetu sisi hii heshima kubwa na ishara ya utambuzi wa juhudi na mchango wa shirika letu katika kujenga jamii na taifa lenye kujali na kusimamia haki na usawa kwa wote. Tunapenda kuchukua nafasi hii pia kukupongeza wewe binafsi na tume nzima kwa uongozi na kazi kubwa ya kukusanya maoni ya Katiba nchi nzima

Aidha Mtandao wa Jinsia unaipongeza Serikali kwa kutoa Uongozi na rasilimali za kuwezesha utekelezaji wa mchakato huu wa kihistoria ambao kwetu ni fursa ya kipekee ya kujenga muafaka wa kijamii na kutengeneza sheria mama itakayoelekeza usimamizi na uwajibikaji juu ya rasilimali zote za nchi yetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

1.2 KUHUSU MTANDAO WA JINSIA
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ni asasi isiyo ya kiserikali yenye lengo la kupigania haki za kijamii, usawa wa jinsia, kukuza uwezo wa wanawake, na kubadilisha mifumo kandamizi kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii. Tangu kuanzishwa kwa shirika mwaka 1993, Mtandao umefanya kazi kubwa katika kuwezesha mjadala wa kijamii na uelewa kuhusu haki na usawa wa jinsia, ukombozi wa wanawake kimapinduzi , kuwajengea wanawake uwezo pamoja na kushawishi mabadiliko ya mitazamo ya kijamii katika ngazi zote kwa kutumia mbinu za uraghbishi, utafiti shirikishi, uchambuzi wa sera , bajeti ya kijinsia , mafunzo ya jinsia kwa wanajamii na watendaji wa ngazi na sekta zote; pamoja na kuandaa na kusambaza taarifa na maarifa. 

Aidha Mtandao wa Jinsia umebuni na kuendeleza majukwaa na fursa za wanajamii kukutana , kujadili , kutafakari na kujenga mikakati ya utetezi na ushawishi kuanzia ngazi za msingi. Hizi ni pamoja na Semina za Jinsia na Maendeleo, Tamasha la Jinsia , Vituo vya Maarifa na Taarifa pamoja na kujenga mashirikiano na masirika na taasisi nyingine katika ngazi ya Taifa, Kikanda na Kimataifa.

Mtandao wa Jinsia unaamini kuwa changamoto nyingi za ubaguzi dhidi ya wanawake zinatokana na mwingiliano kati ya mifumo kandamizi hususan mfumo dume , upepari na utandawazi . Kwa hiyo, juhudi za TGNP za uraghbishi na kujenga nguvu za pamoja zimetokana na chambuzi yakinifu za muktadha wetu wa sasa na tafiti mbalimbali zilizoonesha jitihada za wanawake za kupambana na mifumo kandamizi pamoja na kuonesha hali halisi ya kiwango cha ukiukwaji wa haki za msingi za wanawake katika nyanja zote za uchumi, siasa, na ustawi wa jamii.

Kutokana jitihada hizi , Mtandao wa Jinsia Tanzania ukiunganisha nguvu zake na wanaharakati wengine umetoa mchango katika mijadala ya kitaifa, kikanda na kimataifa kuhusu muktadha wa mfumo wa ubepari , soko huria na athari zake kwa uchumi wa mataifa ya kusini mwa Afrika iliwemo Tanzania. 

Mtandao wa Jinsia umetoa michango katika kujenga hoja ya uzingatiaji wa masuala ya jinsia katika sera, sheria na michakato mbalimbali ya maendeleo hususani ni Bajeti ya Kijinsia , ajira na maisha endelevu, kuainisha mzigo wa kazi wa wanawake kama sehemu muhimu ya mchango wa pato la taifa  utambuzi wa mchango wa wanawake katika uzazi na kupinga vifo vya wanawake katika uzazi, utetezi wa maji safi na salama kama haki ya msingi ya kila mtanzania, utetezi wa ushiriki sawa katika nyanja zote za maamuzi na kupinga aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake na watoto.
KUSOMA ZAIDI BOFYA HAPA


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo