Jaji
Warioba1: Jaji Warioba akiongea na Waandishi wa Habari katika ofisi za
Tume jijini Dar es Salaam leo (Jumamosi, Jan. 5, 2012)
Na Mwandishi Wetu
Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba ametoa ufafanuzi
kuhusu hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa usiku wa mwaka mpya na
kuzungumzia mchakato wa Katiba unaoendelea na kusema Rais hapaswi
kulalamikiwa kwani yote aliyosema yamo ndani ya Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba.
Jaji
Warioba alitoa ufafanuzi huo leo (Jumamosi, Januari 5, 2013) katika
mkutano wake na Waandishi wa Habari wakati akizungumzia tathmini ya kazi
ya kukusanya maoni binafsi ya wananchi kupitia mikutano iliyomalizika
tarehe 19 Disemba mwaka jana (2012).
“Kuna
kitu gani kipya alichosema Rais? Yote aliyosema yapo kwenye Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba na mimi katika mikutano yangu yote nanyi
nimeyaeleza na hakuna asiyejua,” alisema Jaji Warioba ambaye ameshawahi
kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais.
“Rais
alielezea mchakato wote kuanzia kukusanya maoni, kuandaa rasimu,
kufanyika kwa Mabaraza ya Katiba, Bunge Maalum la Katiba na kura ya
maoni…haya yote yapo kwenye sheria ambayo Wabunge waliipitisha,” alisema
Jaji Warioba wakati akijibu swali la Mwandishi wa Habari Jabir Idrissa
aliyetaka kujua kauli ya Tume kuhusu maoni ya baadhi ya wanasiasa kuwa
Rais aliingilia kazi za Tume.
“Hivi
ingekuwaje kama Rais angetoa salam za Mwaka Mpya bila kuzungumzia
mchakato muhimu kwa nchi kama huu wa Katiba,” alihoji Jaji Warioba.
Akizungumzia
mikutano ya kukusanya maoni iliyomalizika mwezi uliopita, Jaji Warioba
alisema kazi ya kukusanya maoni ilianza tarehe 2 Julai mwaka jana na
Tume yake imetembelea na kufanya mikutano 1,776 katika mikoa yote 30 ya
Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa
mujibu wa Jaji Warioba, jumla ya wananchi 1,365,337 walihudhuria
mikutano hiyo na kati yao, wananchi 64,737 walitoa maoni kwa kuzungumza
katika mikutano na wengine 253,486 walitoa maoni yao kwa maandishi
katika mikutano hiyo.
Kwa
mujibu wa maelezo ya Jaji Warioba, takwimu hizi hazijumuishi maoni
yanayoendelea kukusanywa na Tume yake kupitia posta, totuvi ya Tume,
mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu za mkononi ambao hadi
kufikia jana (Ijumaa, Januari 4, 2013) jumla ya ‘sms’ 16,261.
Kuhusu
idadi ya wananchi waliojitokeza mikutanoni na kutoa maoni yao,
Mwenyekiti huyo alisema Tume imeridhika na idadi hiyo na kufafanua kuwa
kilichokuwa kinatafutwa na Tume ni hoja na kwamba haukuwa wakati wa
kupiga kura.
“Ilikuwa
ni muhimu kufikia watu wengi iwezekanavyo na ndiyo maana tumefika kila
sehemu. Lakini tangu awali, tulishasema hatutaweza kumfikia kila mtu,”
alisema na kuongeza kuwa Tume yake imeridhika na idadi na maoni
yaliyotolewa na wananchi na kutoa mfano wa Tume ya Nyalali ambayo
alisema ilipokea maoni ya wananchi 21,000 lakini Ripoti ya Tume hiyo
ilisheheni mambo muhimu kwa taifa.
Jaji
Warioba alifafanua kuwa katika awamu zote nne za mikutano ya kukusanya
maoni, wananchi wametoa maoni kuhusu maeneo yote muhimu kama utawala,
haki, maadili na mamlaka yao na mengineyo.
Aliongeza
kuwa mikutano ya Tume ya kukusanya maoni ililelenga kupata hoja za
msingi ili Tume iweze kuandaa Rasimu ya Katiba ambayo itawasilishwa
katika mikutano ya Mabaraza ya katiba itakayofanyika kila wilaya.
Akizungumzia
hatua inayofuata, Jaji Warioba alisema kuwa kuanzia keshokutwa
(Jumatatu, tarehe 7 Januari, 2013), Tume hiyo itaanza kukutana na
makundi mbalimbali kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu Katiba Mpya.
Makundi hayo ni Vyama vya Siasa; Vyama vya Kitaaluma; Asasi za Kiraia;
Taasisi za Kidini, Vyama vya Wafanyakazi, Wakulima na Wafanyabiashara na
makundi mengine mbalimbali.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti huyo, Tume yake imeshawasiliana na makundi hayo na
imeandaa utaratibu wa kukutana na wawakilishi wao katika ofisi za Tume
na baadhi ya kumbi jijini Dar es Salaam na Zanzibar.
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kazi rasmi Mei 2 mwaka jana (2012) na
kazi ya kukusanya maoni kupitia mikutano imefanyakika kwa awamu nne.
Awamu ya kwanza ilifanyika kati ya Julai 2 – 30, 2012 wakati awamu ya
pili ilifanyika kuanzia tarehe 27 Agosti – 28 Septemba, 2012. Awamu ya
tatu iliyofanyika kati ya terehe 8 Oktoba, 2012 na tarehe 6 Novemba,
2012 na awamu ya nne na ya mwisho ilifanyika kati ya tarehe 19 Novemba –
19 Disemba mwaka jana (2012).