WATOTO WAHAMA KIJIJI WAKIHOFIA KUUAWA

 

 
SIKU moja baada ya Bhoke  Ngariga (45) mkazi  wa Kitongoji cha Senta, Kijiji cha Majimoto wilayani Serengeti kuuawa kinyama kwa kukatwa kwa panga kutokana na mgogoro wa ardhi,  watoto wake wamelazimika kukikimbia kijijini hicho kwa kuhofia nao wanaweza kuuawa.
Ndugu wa marehemu Bhoke wameridhia hilo, hasa baada ya mama yao pia kufariki kutokana na majeraha makubwa aliyopata kutokana na kukatwa mapanga katika mgogoro huo.

Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji hicho, Johannes Masirori alisema kuwa familia hiyo imeondoka Desemba 28 usiku mwaka huu wakiongozana na mwili wa marehemu mama yao.

“Wamebeba kila kitu… Wameahidi hawatarudi tena hapa maana yake wamehamia Kijiji cha Bunchanchari,” alisema.
Kuhusu mifugo waliyokuwa nayo wamekabidhi kwa ndugu zao lakini mizigo ilipakiwa ndani ya gari lililobeba mwili wa marehemu kwenda Bunchanchari.
Alisema hata familia ya mtuhumiwa iliyokuwa inaishi karibu na marehemu Bhoke wamehama, kwa kuwa eneo hilo walikuwa wanaishi kwa ajili ya kilimo na ufugaji na kuwa sasa wamehamia kwenye mji wao ulioko Kitongoji cha Senta. Uchunguzi wa mwili wa Marehemu Bhoke ulifanywa na mganga wa zahanati ya Maji moto, Thomas Wambura chini ya usimamizi wa mkuu wa Kituo kidogo cha Polisi cha Majimoto koplo Deogratias Paul, baada ya gari lililokuwa likimpeleka Inspekta Abdallah Idd ambaye ni Mkuu wa Tarafa ya Ngoreme kuharibikia njiani.
Kwa mjibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji, ng’ombe 35 na mbuzi 20 waliokuwa wameshikiliwa na ndugu wa marehemu wamerejeshwa baada ya ndugu wa mtuhumiwa kulipa Sh160,000 kama gharama za jeneza Sh100,000  na usafiri wa mwili wa marehemu Sh60,000.
Mtuhumiwa Masati mpaka sasa hajapatikana na inadaiwa ametokomea kusikojulikana.
MSINGI WA TATIZO
Ni mgogoro wa ardhi, ambao ulisababisha hadi wakafikishana  baraza la ardhi wilaya, mtuhumiwa alishinda na Bhoke akakata rufaa baraza la ardhi la kata akashinda.

Mtuhumiwa alikata rufaa baraza la ardhi la wilaya Musoma, ambako iliandikwa barua kuwataka watu hao kufika mahakama ya Musoma januari 28,2013 kujadili jambo hilo.
Lakini Desemba 27,2012 wake wa mtuhumiwa walikwenda kulima eneo hilo ambalo lina mgogoro, ndipo ugomvi ulipozuka na kutokea mauaji hayo.
SOURCE:MWANANCHI


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo