Wanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Ardhi
(Aru), kilichopo jijini Dar es Salaam wameandamana mpaka ofisi ya serikali ya
wanafunzi kupinga tangazo lililobandikwa chuoni hapo linalowataka kuanzia kesho
wasivae nguo fupi na za kubana.
Tangazo hilo limebandikwa siku ya Alhamisi wiki
iliyopita, majira ya saa 10 alasiri, likiwa na maandishi yanayosomeka: “kuanzia
tarehe 1 mwezi wa kwanza hakuna mwanafunzi yeyote kuvaa nguo fupi na za kubana.
Tunashukuru uongozi wa wanafunzi kutekeleza hilo kwani tulisikia katika vyuo
vingine sasa zamu yetu.”
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho, Matiko
Chacha, amesema kuwa, baada ya wanafunzi kusoma tangazo hilo waliamua kufanya
maandamano mpaka ofisi ya serikali ya wanafunzi ili kupata uhakika kama wana
taarifa na tangazo hilo na kwa nini hawajashirikishwa.
Amesema kuwa, wao kama serikali ya wanafunzi hawakuwa
na taarifa juu ya uwapo wa tangazo hilo. Hivyo, walishtushwa na ujio wao na kuwajibu
kuwa hakuna kitu kama hicho hata kama lilikuwa labda ni agizo kutoka utawala
lazima lingepita katika ofisi zao.
Wanafunzi hao walimwonyesha kiongozi huyo nakala ya tangazo hilo, ambalo halikuwa na jina wala saini ya mwandishi.
Chacha ameongeza kuwa, amewatuliza wanafunzi hao na
kufikia mwafaka baada ya kulichana tangazo hilo mbele yao na kuwahakikishia
kutokuwapo kwa suala hilo na kuwa, hata kama lingekuwa ni la kweli, lazima
lingepelekwa katika bunge la wanafunzi ili kufanyiwa maamuzi.
Amesema kuwa, ni
vigumu kwa wanafunzi wa chuo hicho kuvaa nguo fupi kutokana na uhalisia wa
masomo yaliyopo kumtengeneza mwanafunzi kuvaa mavazi ya staha, kama vile
suruali.